APRA Tanzania: Kilimo biashara ni fursa kwa wanawake

Imeelezwa kuwa ushiriki wa wanawake katika kilimo biashara kuna mchango mkubwa wa kuwawezesha kukidhi mahitaji yao,pamoja na kushiriki katika mambo mbalimbali ikiwemo kutoa maamuzi ndani na nje ya kaya zao, anaripoti Victoria Kazinja (Diramakini) Morogoro.

Mtafiti mwandamizi kutoka Mradi wa Utafiti wa Sera za Kilimo Afrika (APRA), Dkt.Devotha Kilave, akiwasilisha matokeo ya utafiti uliofanyika katika mikoa ya Singida na Morogoro, juu ya kilimo cha mpunga na alizeti kwa waandishi wa habari. (DIRAMAKINI).

Hayo yamesemwa na Mtafiti Mwandamizi kutoka Mradi wa Utafiti wa Sera za Kilimo Afrika (APRA), Dkt. Devotha Kilave, juu ya utafiti walioufanya katika kilimo cha mpunga na alizeti kwenye mikoa ya Morogoro na Singida, wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti huo kwa waandishi wa habari, katika Chuo kikuu cha Sokoine cha kilimo (SUA) mjini hapa.

Dkt. Kilave amesema kuwa ili mwanamke aweze kuendelea vizuri katika hali halisi ya maisha ya kila siku, kilimo biashara kina mchango mkubwa kuwawezesha wanawake kujikwamua katika umasikini na utegemezi.

Amesema kuwa, ushiriki wa wanawake katika masuala ya kilimo biashara ikiwa ni kilimo cha alizeti au mpunga kuna weza kumuongezea uwezo wa kujiamini katika kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi, kijamii na hata kisiasa.

Amesema, kuna umuhimu wa kumjengea mwanamke uwezo pale majukumu yake ya kila siku yanapoongezeka, kwa kumbadilishia mahusiano yake katika shughuli zake za kila siku na mahusiano yake katika kaya ili kumuwezesha kuwa na uwezo wa kutafuta kipato.

Aidha, amesema kuwa mbali na kilimo cha mpunga kuongezeka lakini anayefaidi zaidi ni mwanaume kwa kuwa na uwezo wa kuamua katika mgawanyo wa fedha zinazopatikana na kwamba umiliki wa ardhi bado uko chini ya mwanaume zaidi kuliko mwanamke.

Hata hivyo, amesema kuwepo kwa umeme katika kijiji au eneo husika kunamuwezesha mwanamke kuweza kuwa na hali nzuri zaidi katika shughuli za uzalishaji za kila siku ikiwemo usindikaji na ukoboaji.

Mkuu wa Mradi wa APRA Tanzania, Prof. Aida Isinika. (DIRAMAKINI).

Kwa upande wake Mkuu wa Mradi wa APRA Tanzania, Prof. Aida Isinika amesema kitendo cha wanawake kuendesha kilimo biashara kumewawezesha kuzalisha mazao kwa tija na kuwawezesha kujikimu katika maisha yao na kuwapa nafasi ya kushiriki mambo mengine ya maendeleo ikiwemo siasa.

Utafiti wa zao la alizeti umefanyika katika Mkoa wa Singida kwenye wilaya mbili za Iramba na Mkalama huku utafiti wa mpunga ukifanyika katika Mkoa wa Morogoro kwenye bonde la mtoKilombero Tarafa ya Mngeta.

No comments

Powered by Blogger.