CMSA yawataka wawekezaji kuwa makini na fursa za mitandaoni

Wawekezaji nchini Tanzania wametakiwa kuwa makini na fursa za uwekezaji zinazotangazwa kiholela kwa njia ya mitandao ambazo hazijaidhinishwa na mamlaka husika za usimamizi wa uwekezaji ili kuepusha kutapeliwa, anaripoti Mwandishi Diramakini (diramakini@gmail.com) Dar es Salaam.

Wito huo umetolewa mapema leo Oktoba 5,2020 jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama katika uzinduzi wa Wiki ya Wawekezaji katika Masoko ya Mitaji Duniani.

Amesema kuwa, CMSA inaadhimisha wiki hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya masoko ya mitaji kwa kuendesha kampeni ya kutoa elimu kwa makundi mbalimbali na umma kuanzia Oktoba 5 hadi 9, mwaka huu ili kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu masoko ya mitaji na uwekezaji.
Aidha, amesema, uzinduzi huo ni sehemu ya utekekelezaji wa mpango mkakati wa CMSA wa miaka mitano 2018/2019 hadi 2022/2023 ambao unapanga kuendeleza sekta ya masoko ya mitaji Tanzania kwa kutoa elimu na kuongeza uelewa kwa makundi mbalimbali na kupanua wigo wa washiriki na kujenga uwezo kwa watendaji katika masoko ya mitaji kulinda maslahi ya wawekezaji.

"Kwa kuzingatia kuwa Tanzania inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda mahitaji ya mitaji kwa shughuli za uchumi yanaongezeka hivyo ni vyema kujenga uwezo na ushirikiano wa pamoja na wadau wakuu wa sekta ya masoko ya mitaji utawezesha wahitaji mitaji ya kifedha,"amesema CPA Mkama.

Ameongeza kuwa, mpaka sasa uwekezaji katika masoko ya mitaji ni shilingi trilioni 27ambapo uwekezaji katika hisa ni trilioni 15 hati fungani trilioni 11.5 na mifuko ya uwekezaji wa pamoja ni bilioni 500.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (UTT-AMIS), Simon Migangala amesema, kwa miaka michache uwekezaji umeongezeka hadi kufikia wawekezaji 12,000 ambapo ukuaji ulikuwa haujazidi milioni 22 na sasa ukuaji umefika hadi milioni 122.

Hata hivyo, amesema katika kuadhimisha Wiki ya Wawekezaji Duniani watatumia vyombo vya habari kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika masoko ya mitaji pamoja na faida zake.

Post a Comment

0 Comments