EWURA CCC yatoa wito kwa watumiaji, watoa huduma nishati na maji

Watumiaji na watoa huduma za nishati na maji Manispaa ya Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla wamesisitizwa kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuzidi kuimarisha uhusiano na ufanisi wa huduma baina ya pande zote mbili,anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA CCC) Mkoa wa Mara, Robinson Wangaso wakati akitoa semina kwa wahudumu wa afya ya msingi ngazi ya jamii Manispaa ya Musoma iliyofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Musoma.

Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA CCC) Mkoa wa Mara, Robnison Wangaso akitoa semina kwa wahudumu wa afya ya jamii ngazi ya msingi Manispaa ya Musoma. Semina hiyo imefanyika Ukumbi wa Manispaa ya Musoma Oktoba 16, mwaka huu. (DIRAMAKINI).
Ambapo lengo la semina hiyo ni kuwajengea uelewa mpana kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwemo haki na wajibu wa watumiaji wa nishati, pamoja na watoa huduma.

Katika semina hiyo, Wangaso amesema, baraza hilo limekuwa na utaratibu wa kukutana na watoa huduma na watumiaji kutoka makundi mbalimbali ikiwemo wajasiriamali, wafanyakazi,wahudumu wa wfya na wananchi kwa lengo la kuwapa elimu ikiwa ni utekelezaji wa majukumu ya baraza hilo kama ambavyo limeundwa chini ya kifungu cha 30 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji sura ya 414.

Amebainisha kwamba, EWURA CCC ina wajibu wa kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa maji na nishati kama ilivyo dhamira ya kuanzishwa kwake, sanjari na kuhakikisha inapokea malalamiko na kero mbalimbali za watumiaji wa huduma za nishati na maji na kuweza kuzipatia ufumbuzi kwa maslahi mapana ya pande zote mbili yaani watumiaji na watoa huduma.

"Ni wajibu wa mtumiaji wa huduma iwapo ana kero kuziwasilisha EWURA CCC kwa maandishi, ambapo tutaita pande zote mbili na kufanya usuluhishi, ili kila pande ipate haki lengo ni kuwezesha mtumiaji kupata huduma bora na mtoa huduma kupata manufaa kutokana na ubora wa huduma yake anayoitoa, mtu anapokuwa na kero cha kwanza amweleze mtoa huduma ikishindikana alete malalamiko yake EWURA CCC na si kwenda Polisi ama sehemu nyingine lengo kupata usuluhishi wenye tija," amesema Wangaso.

Winfrida Bihemo Mjumbe wa EWURA CCC Mkoa wa Mara akitoa mada katika semina hiyo, kuhusiana na ufahamu juu ya haki na wajibu wa mtumiaji wa huduma amesema kuwa, mtumiaji wa huduma za nishati na maji ana haki ya kuelimishwa, haki ya kufidiwa iwapo amepata hasara kutoka na huduma aliyotumia, kulalamikia huduma iwapo haikidhi ubora, kupewa mwongozo wa utatuzi migogoro.

Pia Bihemo ameongeza kuwa, mtumiaji wa huduma ana wajibu kulipia ankara ya huduma aliyopewa kwa wakati, kutunza miundombinu ya huduma iweze kuwa endelevu, kutoa taarifa akigundua bidhaa anayotumia iwapo ina kasoro, pamoja na kufuata taratibu na makubaliano ya mkataba wa huduma wakati wote bila kukiuka.

Kwa upande wake Afisa Msaidizi Utawala na Huduma kwa Wateja EWURA CCC, Mkoa wa Mara, Denis akiwasilisha mada kuhusiana na kanuni za ubora wa huduma za maji na usafi wa mazingira amesema kuwa, kwa mujibu wa kanuni ya 16 (1) ukaguzi na upimaji wa mita unapaswa ufanyike mteja akiwepo eneo huska ili kuondoa malalamiko.

Wahudumu wa afya ya msingi ngazi ya jamii Manispaa ya Musoma wakiwa kwenye semina iliyoendeshwa na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA CCC) Mkoa wa Mara. Semina hiyo imefanyika Oktoba 16, mwaka huu Ukumbi wa Manispaa ya Musoma.(DIRAMAKINI).
Pia amesisitiza kuwa, mteja akikatiwa huduma kimakosa ikiwemo maji atakuwa na haki ya kulipwa fidia kwa mujibu wa kanuni ya 29 (1) sambamba na kurejeshewa huduma ndani ya saa 24 iwapo mteja atalipa deni lililopelekea akatiwe huduma kwa mujibu wa kanuni ya 31( 1).

"Utaratibu wa kulipa ankara kwa mujibu wa kanuni ya 23 (1) mteja anatakiwa kulipa ankara yake ndani ya siku 30 kutokea pale alipopokea ankara yake kama hatakuwa na uwezo ni wajibu wake kufika sehemu husika na kutoa taarifa, tunahitaji elimu hii iwafikie wananchi wote kusudi watambue wanapolipia kwa wakati huduma inamsaidia mtoa huduma kupanua wigo wa huduma yake kwa watu wengine tena,"amesema Danu.

Erasto Kisha kutoka Makao Makuu ya EWURA CCC jijini Dar es Salaam amewataka waliohudhuria mafunzo hayo kuhakikisha wanakwenda kuyatumia kwa faida ikiwemo kuwaelimisha wengine ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria, huku akibainisha kuwa wamejipanga vyema kupeleka elimu hiyo mpaka ngazi ya chini maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wao washiriki wa semina hiyo, James Matiko na Paul Mussa wakazi wa Manispaa ya Musoma wakizungumza kwa nyakati tofauti na Diramakini wamesema, elimu waliyoipata imewapa mwanga, ambapo masuala mengi hawakuweza kuyajua kabla ya semina hiyo.

Wamesema,kwa sasa wamefahamu kutokana na fursa ya kuuliza maswali mbalimbali na kupewa majibu kutoka kwa watoa huduma na nishati na maji, huku wakiahidi kwenda kuwa mabalozi wema wa kuwaelimisha wananchi wengine katika majukumu yao ya kila siku.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news