Ruvuma watajwa kuwa na hazina ya tani milioni 227 za makaa ya mawe

Shughuli za utafiti na uchimbaji wa makaa ya mawe katika Mkoa wa Ruvuma zinafanyika katika Wilaya ya Mbinga maeneo ya Mbalawala na Mbuyula, Wilaya ya Songea katika maeneo ya Muhukuru, Njuga na Mtyangimbole na Wilaya ya Nyasa maeneo ya Malini Kata ya Mtipwili na Mbambabay, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati akikagua uzalishaji wa makaa ya mawe kutoka mgodi wa Ngaka wilayani Mbinga mkoani Ruvuma hivi karibuni.

Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Jumanne Mohamed Nkana amesema Mkoa wa Ruvuma una hazina ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 227 ambayo yanatarajiwa kuchimbwa kwa miaka 300.

Kulingana na Nkana,tafiti za awali za makaa ya mawe zimefanyika katika maeneo ya Mbalawala Mbinga ambako imebainika kuwa na tani milioni 99.5, Mbuyula Mbinga tani milioni 15.1 na Muhukuru Songea tani milioni 27.

Mgodi wa makaa ya mawe Malini Mbambabay Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.

Kwa mujibu wa Nkana tafiti katika eneo la Njuga wilaya ya Songea kuna tani milioni 23, wilaya ya Nyasa maeneo ya Malini tani kata ya Mtipwili milioni 29, kijiji cha Liweta Kata ya Mbaha tani milioni 34.Amesisitiza kuwa, ubora wa makaa ya mawe yanayopatikana kwenye maeneo hayo yana wastani wa Calorific Value (CV)5,000 hadi 7,000.

Hata hivyo Afisa Madini Mkazi huyo wa Mkoa wa Ruvuma amesema uchimbaji mkubwa wa makaa ya mawe unafanyika katika maeneo ya Mbalawala,Mbuyula, Mbambabay, Muhukulu na Liweta.

Amewataja wateja wakubwa wa makaa ya mawe yanayochimbwa katika maeneo hayo kwa sasa kuwa wapo ndani ya nchi na katika nchi jirani za Rwanda, Kenya na Uganda na kwamba wanatarajia kuanza kuuza makaa ya mawe katika nchi ya India.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ameziagiza kampuni zinazochimba makaa ya mawe mkoani humo kuuza makaa ya mawe kwenye viwanda vya ndani ili kupata nishati ya kutosha na ziada inayobaki isafirishwe kwenda nje ya nchi.
Mndeme pia ameziagiza kampuni hizo kutoa ajira kwa Watanzania ili waweze kunufaika na rasilimali za nchi huku akisisitiza kuchimba makaa ya mawe yenye viwango ili soko lipanuke, na kuzingatia usalama na afya za watumishi wote wanaofanya kazi katika migodini.

Maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Magufuli kuzuia kuagiza makaa ya mawe toka nje,badala yake watumiaji wote kutumia makaa ya mawe ndani ya nchi,hususani toka mkoani Ruvuma yamesababisha soko la makaa hayo kupanda na kutoa ajira kwa watanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news