RUWASA yakumbushwa kuzijengea uwezo Jumuiya za Watumiaji Maji nchini

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imetakiwa kuhakikisha Jumuiya za Watumiaji Maji (CBWSOs) zinakuwa na uwezo wa kupanga, kukusanya na kusimamia maduhuli yatokanayo na mauzo ya maji ili kuwa na miradi endelevu, anaripoti Mohamed Saif, Mwanza.
Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Profesa Idrissa Mshoro akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maofisa wa RUWASA kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Pwani na Simiyu (hawapo pichani).
Maelekezo hayo yalitolewa hivi karibuni mkoani Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Profesa Idrissa Mshoro wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha maofisa wa RUWASA kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Pwani na Simiyu.

Profesa Mshoro amesisitiza kwamba ili miradi inayotekelezwa na RUWASA iwe endelevu ni lazima Jumuia za Watumiaji Maji (CBWSOs) wakajengewa uwezo kuanzia hatua za awali.

“Menejimenti mnatakiwa kuimarisha uwezo wa jumuiya kwa mipango madhubuti ya kujenga uwezo, kudhibiti na kusimamia taasisi na huduma, CBWSOs ziwe na uwezo wa kupanga, kukusanya na kusimamia maduhuli yatokanayo na mauzo ya maji yatakayowezesha uendeshaji na matengenezo ya mradi,”amesisitiza Profesa Mshoro.

Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Profesa Idrissa Mshoro (katikati) na watendaji wa RUWASA wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Mkama Bwire (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maofisa wa RUWASA kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Pwani na Simiyu.
Amewaelekeza watendaji wa RUWASA kuhakikisha wanaimarisha uhusiano na ushirikiano na taasisi zingine zikiwemo Ofisi za Mabonde, Mamlaka za Maji, Ofisi za Serikali za Mitaa, Halmashauri na Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Mikoa ili kufikia malengo na mipango walionayo.

Amesema, kumekuwa na changamoto kwa halmashauri kutopata taarifa za RUWASA kama inavyopasa na hivyo ameelekeza watendaji kuhakikisha wanawasilisha ripoti zao kwenye Ofisi za Halmashauri na Mikoa na Wilaya kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Profesa Idrissa Mshoro (wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja na watendaji walioshiriki kikao kazi cha Maofisa wa RUWASA kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Pwani na Simiyu.
Mbali na hilo, Profesa Mshoro ameitaka Menejimenti ya RUWASA kuonesha njia kwa kudumisha dhana ya ushirikiano katika ngazi ya mipango, bajeti na mawasiliano na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji.

“Undugu huo wa uasili na usambazaji wa rasilimali maji unafanya kusiwe na mjadala katika umuhimu na ulazima wa kushikiana kwa taasisi hizi, tutumie fursa ya mtazamo, msimamo na msisitizo wa Wizara ya Maji katika ufanyaji kazi kama wizara moja, huduma moja, mlengwa mmoja,”amelekeza Profesa Mshoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news