Safari ya maisha ni fumbo, usigeuke mwiba, kuwa faraja kwao

Safari ya maisha yetu, imeghubikwa na vigingi vingi. Vigingi vya kuzima taa za tuelekeapo ili pawe giza tusifike na wakati mwingine vya kuhitimisha kabisa mwendo wetu, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Ni sahihi kusema kuwa, safari ya maisha yetu ni fumbo, maana hakuna anayejua huko aelekeako atakutana na nini, nani au ataifikia lini hiyo hatima.

Ndiyo maana ni jambo jema sana kuhakikisha kabla na baada ya kutaka kuanza safari yako umshirikishe Mungu hitaji na tamanio lako la huko uendako. Ulimwengu wa sasa una makundi mawili ya binadamu ambao wanaweza kuwa faraja kwako au kilio kwako.

Mosi kundi la wenye huruma, upendo na pili kudi la wenye jicho la husda, hatua kwa hatua tuangalie namna ya kuyasoma makundi haya na namna ya kukabiliana nayo.

Wenye husda wanatamani kutumia kila upenyo kukuangusha.(Elitethrive).

Tunapozungumzia kundi la kwanza la watu wenye huruma na upendo, hawa ni wale ambao hawawezi kukuacha uanguke, wenye kutamani safari yako iwe ya heri na mafanikio tele ambao bila kutegemea chochote kutoka kwako, wao wapo tayari kukuombea na kukutia moyo katika magumu yote unayopitia.

Ni kundi ambalo linaweza kukufanya machungu uliyonayo ukayageuza kuwa faraja na kuendelea na safari. Kundi hili, au watu wa namna hii ni wema, yafaa uwashikilie, uwaombee na ujumuike nao katika kupiga mwendo wa safari yenu.

Kwani ikiwa ni katika biashara, kazini au katika mambo ya kifamilia wanaweza kukuonyesha njia hadi kufikia ndoto za maisha yako.

Kwa upande wa kundi la pili ambalo ni la wenye jicho la husda, hawa unapaswa kujichunga nao, kataa kuwashirikisha mipango yako, ikiwezekana jitenge nao, lakini kikubwa zaidi ishi nao kwa akili.

Watu wa namna hii, huwa na vitabia vya ovyo ovyo, kila unalolifanya kwao kwa mtazamo wa nje watakuonyesha kuwa ni jema, lakini ukigeuza kisogo ulilolifanya na kufanikiwa watalitengenezea tanuru la moto, mwisho wa siku watakusukuma kabisa, ukidondoka ndiyo faraja yao.

Aina hii ya watu wapo sana katika maeneo yetu ya biashara, jamii na kazi zetu au ofisini kila siku, usipojipa nafasi na kujiingiza mzima mzima watakuangusha na utabakia mkiwa, usijipe imani nao sana maana ni kati ya watu ambao wanaweza kutengeneza ukweli kuwa uongo na uongo kuwa ukweli.

Matokeo yake, utaonekana wewe ni kati ya watu ambao hawafai kabisa katika nafasi au kazi unayotekeleza. Ili kuwashinda watu hawa ishi nao kwa akili, usiwape nafasi ya kukusoma ili watimize takwa lao la kuteka fikra zako hadi kukuangusha.

Tuzingatie kuwa, safari yetu ya maisha ya kila siku inakuwa ya baraka tu pale ambapo tutamshirikisha Mungu kila jambo badala ya kuyaanika mambo yako kwa watu, ni tumaini langu kuwa, safari yako ya sasa unaweza kutambua namna ya kupiga hatua ili kufanikiwa pasipo utegemezi wa mwanadamu kwa kuwa, tamanio na malengo yako mwenye uwezo wa kukuheshimisha ni Mungu pekee. Tukutane wakati mwingine hapa. Pia akikisha unakuwa faraja kwa wengine, ili kila mmoja aweze kujifunza na kukutolea ushuhuda mwema popote uingiapo na utokapo.

No comments

Powered by Blogger.