Usijiingize mzima mzima, jipe muda

Maisha yanakwenda mbio mno. Kila panapo kucha wengi wetu tunatamani kutajwa miongoni mwa watu ndani ya jamii wenye mafanikio makubwa, bila kujua katika hayo mfanikio kuna hatua za kuyafikia, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Acha kujiingiza mzima mzima, jipe muda wa kutafakari ni kanuni zipi sahihi za kukuwezesha kuyafikia malengo yako ili uweze kupiga hatua kihalali katika maisha pia usikimbilie kupanda ngazi ambayo  uwezo wa kuipanda kwa kasi hauna, panda taratibu hadi ufike mwisho.

Miongoni mwa kanuni hizo za kukuwezesha kufanikiwa katika maisha yako ni pamoja na kusoma alama za nyakati katika mazingira yanayokuzunguka,baada ya kujitambua wewe ni nani katika hiyo jamii.

Ninaposema, unapaswa kujitambua wewe ni nani katika hiyo jamii ninamaanisha kuwa, uwepo wako hapo ulipo una umuhimu mkubwa sana bila kujali kiwango chako cha taaluma au uduni wako katika hali ya kipato au pengine kiuchumi.

Ukishajitambua wewe ni nani unaweza kuziona fursa zilizopo hapo, kwani bila kuangalia uwezo wako wa kitaaluma au aina ya maisha unaweza kuvumbua jambo jipya, baadae likawa faraja kwa wengine.

Utajisikiaje ukiona unafanya jambo ambalo lilionekana kuwa la kawaida au la aibu kwa sababu ya hulka au imani za wengi, halafu baadae likainua viwango vyako vya maisha.

Mfano mdogo, hapo ulipo umekaa miaka na miaka unazunguka huku na kule kusaka ajira, lakini haujabahatika kuipata. Huku kila ukiamka asubuhi, unapoishi wengi wa wanajamii wanatamani kupata kifungua kinywa kwa ajili ya kuendelea na harakati za maisha, bila kujali jinsia yako ukaamua kuwa, sasa ninajitosa rasmi kuuaga umaskini.

Kwa namna gani, unaamua kujiingiza katika uchuuzi wa vitafunwa ili uweze kuziba pengo la mahitaji ya jamii inayokuzunguka, kwa sababu mahitaji yao ni ya mapema asubuhi, nawe ukaamka mapema na kuandaa vitafunwa hivyo, tena vya moto kabisa na vyenye ubora kwa ajili ya kukidhi mahitaji hayo na ikiwezekana ukawawekea na chai bila kujali umeweka meza nje au haujaweka.

Unadhani nini kitatokea iwapo huduma yako itakuwa bora, kwanza utakuwa umewawezesha wanajamii kupata huduma rahisi na ya haraka kwa mapema, hivyo wale ambao walikuwa wanategemea kula vitafunwa vilivyolala watakuwa hawavihitaji tena, bali watakuwa wanakutegemea wewe ili uweze kuwaandalia.

Mategemeo yao kwako, ndiyo faida yako ya kuinuka kiuchumi. Kwani, kadri mahitaji yatakavyokuwa yanaongezeka nawe utajitengenezea kipato cha kuyaendea malengo yako makubwa katika maisha yako ya kila siku. Jambo la msingi ni kuweka uaminifu, kuheshimu rika zote, kuweka unyenyekevu mbele ili kuwavuta wengi.

Huo ni mfano mmoja, lakini kupitia mfano huo unaweza kuutumia kwa kila unachoamini unaweza kukifanya katika jamii inayokuzunguka kikabadilisha historia ya maisha yako, huu ni wakati wetu wa kubadilika na kujikita zaidi katika kujitegemea kuendesha mambo yetu kwa manufaa yetu na familia zetu ya sasa na baadae.

Tusikubali kuwa tegemezi katika kazi za watu, hizo hazitakuwezesha kufikia kilele cha mafanikio katika maisha yako, bali kuwa wabunifu na kujiwekea mazingira ya kujitegemea wenyewe ili kuupiga teke umaskini.

Mara nyingi, unapotaka kufanya uamuzi wa busara namna hii unaweza kukumbana na vikwazo vingi, ila moja ya sifa kuu ya kuvishinda ni kuvipa kisogo na kusonga mbele, anzia popote ulipo, lazima upige hatua, usikubali kukata au kukatishwa tamaa. Uvumbuzi wetu ndiyo faraja ya kutupeleka katika vilele vya mafanikio muda wowote.

Usimwangalie yeye anapanda vipi katika ngazi,tumia mbinu na maarifa yako kupanda mwenyewe lazima ufanikiwe hata kama utapanda taratibu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news