Plan International yakutanisha wadau kupinga ukatili

Shirika la Plan International Mkoa wa Geita limekutanisha katika mdahalo,mashirika yasiyo ya kiserikali,madhehebu ya dini,vyombo vya ulinzi,vyombo vya habari, viongozi wa serikali na wadau wengine ili kujadili na kuweka mkakati wa kupambana na ukatili wa kijinsia,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.

Meneja wa Plan International Mkoa wa Geita, Adolf Kaindoa amesema kuwa lengo la mdahalo huo uliofanyika katika Ukumbi wa Magufuli katika Kituo cha EPZA Geita ni kuweka mikakati ya pamoja ili kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ili Mkoa wa Geita kuwa mkoa salama kwa wanawake na watoto.


Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel (katikati) akimsikiliza Meneja wa Plan International Mkoa wa Geita, Adolf Kaindoa katika Dawati Maalum la Jinsia katika Ukumbi wa Magufuli Kituo cha EPZA Mjini Geita katika mdahalo wa ukatili wa kijinsia (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa, ukatili wa kijinsia katika mkoa huo umeongezeka na kufikia asilimia 64 na kusababisha mkoa huo kushika nafasi ya tano nchini kwa vitendo vya ukatili wa kimwili.

Aidha, ameongezea kuwa, mkoa huo uko nafasi ya 10 kitaifa katika vitendo vya mimba za utotoni kwa wastani wa asilimia 30.


Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel (kushoto) akiteta jambo na Meneja wa Plan International Mkoa wa Geita, Adolf Kaindoa wakati wa mdahalo wa ukatili wa kijinsia uliofanyika katika Ukumbi wa Magufuli katika Kituo cha EPZA Mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Meneja wa Plan International Mkoa wa Geita, Adolf Kaindoa amesema shirika hilo limetumia siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kukutanisha wadau mbalimbali ili kupata mikakati ya pamoja kupambana na ukatili huo.

Kwa upande wake Mwanasheria kutoka kituo cha Msaada ka Kisheria cha Himiza, Penina Mashimba amesema kuwa, vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia kwa mujibu wa Sheria za Tanzania ni makosa ya jinai hivyo mtu anayetenda ukatili huo anaweza kupata adhabu mahakamani ikiwa ni pamoja na kufungwa jela au faini inayofikia milioni tano.

Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Matha Mkupasi amesema jamii inapaswa kuelimishwa ili katika mapambano ya ukatili wa kijinsia yaweze kufanikiwa.

Amesema kuwa, baadhi ya wazazi wanahusika katika ukatili wa wanawake na watoto huku akitoa mfano kwa wazazi wanaoshawishi watoto kuacha shule ili waende kuolewa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyang'hwale, Mariam Chaurembo ameshauri wadau mbalimbali wanaotoa elimu kwa jamii kuhusu kutokomeza ukatili wa kijinsia kujikita zaidi kwa watu wa chini hasa wazazi ili waweze kujengewa uelewa kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia.

Chaurembo amesema, wazazi wakipata elimu kuhusu ukatili wataweza kupeleka watoto shule kama vile watoto wa kike kukaa hosteli ili kumkinga mtoto wa kike kupata mimba za utotoni na kuacha masomo.


Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel (wa pili kushoto) wa kwanza ni Meneja wa Plan International Mkoa wa Geita, Adolf Kaindoa,kulia ni Matha Mkupasi Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe wakiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali walioshiriki mdahalo wa ukatili wa kijinsia katika Ukumbi wa Magufuli katika kituo cha EPZA Mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).

Wadau mbalimbali katika mkoa wa Geita walikutanishwa pamoja na Shirika la Plan International katika mdahalo wa pamoja kujadili na kupata mikakati ya pamoja ya kuwawezesha kupambambana na kuondoa ukatili dhidi ya mwanamke na mtoto katika mkoa huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news