Azam FC yasonga mbele Kombe la Shirikisho

Wanalambalamba, Azam FC imesonga mbele Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Magereza,anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mabao ya Obrey Chirwa dakika ya 24 na Never Tigere dakika ya 65 Desemba 26, 2020 katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam yalifunga hesabu.

Azam FC walionekana kuugawa mchezo kwa vipindi viwili ambapo kipindi cha kwanza Obrey Chirwa alipachika bao hilo kwa kichwa akitumia kona ya Never Tigere.

Pia kipindi cha pili Azam FC ilipata bao kupitia kwa Ner Tigere ambaye amekuwa nyota wa mchezo huo akihusika kwenye mabao yote mawili, akifunga bao la pili na kutoa pasi moja ya bao.

Taji la Kombe la Shirikisho kwa sasa lipo mikononi mwa Klabu ya Simba ambao leo Desemba 27, 2020 watakuwa na kazi ya kuanza kutetea kikombe hicho mbele ya Majimaji ya Songea, Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mechi nyingine za FA zitakazopigwa leo ni pamoja na Namungo FC dhidi ya Green Warriors na Mtibwa Sugar itakabiliana na Geita Gold.

Hata hivyo, mshindi wa Kombe la FA huwakilisha nchi kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo kwa msimu huu Namungo FC kutoka Lindi ndio wanaiwakilishi Tanzania, na matokeo yao yamekuwa ya kuvutia.

Post a Comment

0 Comments