Diwani Kata ya Mzimuni aanza kutekeleza Ilani

Ahadi zilizotolewa kwenye majukwaa kwenye kampeni za uchaguzi katika maeneo mbalimbali Kata ya Mzimuni jijini Dar es Salaam tayari zimeanza kutekelezwa mara moja, ambapo tayari miundombinu ya wanafunzi kupata chakula imeanza kushughulikiwa kwani haikuwepo awali, anaripoti Mwandishi Diramakini (Dar es Salaam).

Akizungumza na Mwandishi Diramakini jijini Dar es Salaam, Diwani Mpya Kata ya Mzimuni, Manfred Lyoto amesema kuwa ni kweli taratibu zimeanza kufanyika kwa ajili ya wanafunzi kupata chakula, lakini kuna baadhi ya changamoto ambazo itabidi zishughulikiwe.

"Kama tulivyoahidi kuhusu wanafunzi wetu kupata chakula taratibu zinaendelea, tunachotakiwa kwanza tunaweka vizuri miundombinu kutokana na kwamba awali haikuwepo kwa sababu hata hicho chakula kilikuwa hakipikwi,"amesema Diwani Lyoto na kuongeza;

"Mfano hakuna jiko, wapishi, eneo la kupikia, vyombo lakini pia lazima chakula hicho kwa watoto wetu kiandaliwe katika mazingira mazuri na yenye usalama,"amesema.

Kuhusu kuweka uzio katika shule za kata hiyo amesema, changamoto iliyojitokeza ni kwamba tathmini ya gharama zilizofanyika awali kama miaka mitatu iliyopita zilikuwa ni ndogo tofauti na sasa ambapo hata gharama za saruji zipo juu zaidi.

"Kwa hiyo tunaweka kuchelewa kidogo kumaliza tofauti na jinsi tulivyokuwa tumepanga kwamba tutamaliza haraka,"amesema Diwani.

Aidha, amesema zoezi la kupima tayari hivi sasa wataalam wanaendelea na tathmini ya kujua ni kiasi gani kitatumika katika kufanya shughuli ya kuweka fensi.

Diwani Lyoto amewaomba wanachama na wapenzi wa CCM kutoa ushirikiano kwa viongozi waliowachagua ili waweze kufanya kazi kwa weledi mkubwa zaidi na badaye kuweza kufikia malengo kama walivyoahidi wakati wa kampeni mbele ya wananchi hao.

"Lakini wananchi na wanachama pia wanatakiwa kujua kwamba wakati huu ni wa kumuunga mkono Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kauli yake ya 'Hapa Kazi Tu' kwa maendeleo ya nchi yetu na Taifa kwa ujumla, uchaguzi umeisha maana yake tumeumaliza kwenye majukwaa sasa tufanye kazi,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news