Hope for Girls and Women Tanzania lataka watoto wa kike wasiachwe nyuma kielimu

Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) linalojihusisha na kutoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni mkoani Mara limetoa wito kwa wazazi na walezi kuwapa kipaumbele cha elimu watoto wa kike kwani wana nafasi ya kuleta mapinduzi chanya ya maendeleo katika jamii yao na Taifa kwa ujumla, anaripoti Amos Lufungilo (Diramakini) Mara.
Wasichana kutoka kituo Cha Nyumba Salama kinachomilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania wakiimba katika hafla hiyo iliyofanyika Shule za Amani Manispaa ya Musoma.(Picha na DIRAMAKINI).

Hayo yamesemwa leo Desemba 23, 2020 na Afisa Uhamasishaji Jamii kutoka shirika hilo, Emmanuely GoodLuck kwa niaba ya Mkurugenzi wa shirika hilo, Rhobi Samwelly wakati akizungumza na DIRAMAKINI kando ya mkusanyiko wa hitimisho la kambi ya watoto wanaohudumiwa na Shirika la FORM chini ya Mkurugenzi wake, Samwelly Mpanilehi, ambapo hitimisho hilo limeambatana na kuwafanyia sherehe ya Krismas watoto hao katika Shule za Amani Manispaa ya Musoma.

Hafla hiyo imeandaliwa na FORM na kuwajumuisha wasichana kutoka Kituo cha Nyumba Salama walioalikwa na Kituo cha Jipe Moyo na wameweza kutoa shuhuda mbalimbali walivyoishi, huku pia wasichana kutoka Kituo cha Nyumba Salama kinachomilikiwa na Shirika la HGWT wakipata fursa ya kutoa shuhuda jinsi walivyokimbia ukeketaji na kuokolewa na shirika hilo na kuweza kuendelezwa kielimu katika kuhakikisha kwamba wanafikia malengo yao.

GoodLuck amesema, jamii inawajibu wa kuwapa kipaumbele watoto wa kike kwa kuwasomesha badala ya kuwapa fursa hiyo watoto wa kiume peke yao, amehimiza kuwathamini sambamba na kuhakikisha haki zao za msingi zinalindwa na kuheshimiwa katika kuandaa kizazi chenye manufaa kwa siku za usoni.

"Elimu ndio urithi pekee kwa watoto, tusiwabague watoto wa kike katika kuwapa elimu. Serikali imeendelea kupinga ukatili wa kijinsia muda wote na sisi kama Hope tutashirikiana juhudi hizo. kutowasomesha watoto wa kike ni kuwafanyia ukatili naomba kila mwananchi ashiriki kikamilifu kupinga ukatili na kupigania haki za watoto wa kike ikiwemo kuwasomesha hasa kipindi hiki ambapo waliofaulu watajiunga na kidato cha kwanza ili kuwaandalia maisha bora na kulitumikia Taifa kwa siku za usoni,"amesema GoodLuck.

Aidha, ameongeza kuwa, shirika hilo linaendelea kutoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji pamoja na kuwapa hifadhi wasichana wanaokimbia ukeketaji kupitia Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari na Nyumba ya Matumaini Mugumu Serengeti ambapo kwa sasa zaidi ya wasichana 300 wanahifadhiwa katika vituo hivyo wakikimbia kukeketwa msimu huu. 

Nao Mariam Ryoba na Veronica Lucasa wanaohifadhiwa Nyumba Salama Kiabakari wakitoa ushuhuda mbele ya wazazi na viongozi wa Serikali waliohudhuria hafla hiyo, wamemshukuru Mkurugenzi wa HGWT, Rhobi Samwelly kwa namna alivyowasaidia kuwapa hifadhi walipokimbia ukeketaji kutoka katika familia nao na kuwaendeleza kielimu ambapo kwa sasa wamehitimu darasa la saba na kufaulu kujiunga na kidato cha kwanza.
Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Pharles Kisena akizungumza katika hafla hiyo ambapo alikuwa mgeni rasmi.(Picha na DIRAMAKINI).

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Askofu Pharles Kisena aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amewatia moyo wasichana wanaoishi Nyumba Salama na Jipe Moyo kuendelea kumtumaini Mungu na kutokata tamaa katika maisha yao, huku akipongeza taasisi zote zinazosaidia watoto dhidi ya ukatili kuendelea kufanya hivyo kwa upendo.

Aidha, Askofu Kisena ameitaka jamii kuishi kwa kutenda matendo mema yenye kumpendeza Mungu na kuwasaidia wenye uhitaji katika jamii ili kutimiza upendo ambao umeagizwa na Kristo kupitia kitabu Kitakatifu cha Biblia sambamba na kuishi kwa kutimiza wajibu na kutenda haki kwa kila mmoja kulingana na nafasi yake anayoitumikia.

Akisoma risala ya Shirika la Faraja Orphans Rescue Ministry (FORM), Mwalimu Emmanuely Mtatiro amesema kuwa, shirika hilo limekuwa likiwasaidia watoto yatima na waishio mazingira magumu tangu lilipoanzishwa miaka 15 iliyopita, limefanikiwa kujenga shule za awali na msingi kuendelea kuwalipia matibabu, kuwaendeleza wanafunzi linaowahudumia katika vyuo vya ufundi, ambapo tangu limeanzishwa limeweza kuwasaidia watoto 75.

Post a Comment

0 Comments