Kamati ya Bunge yapitisha Sheria kali kwa watoto China

Gazeti la China Daily limeripoti kuwa mtoto mwenye umri wa miaka 12 anaweza kutiwa hatiani na kukabiliwa na mashtaka ya jinai iwapo atafanya makosa ya uhalifu kwa makusudi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
(Picha na CNN)

Hayo yanajiri baada ya marekebisho ya sheria kupitishwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa baada ya kujadiliwa kwa mara ya tatu.

Sheria hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia Machi Mosi, 2022 na inahusisha watoto wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 14.

Wachambuzi wa masuala ya kisheria wanasema, hatua hiyo inamaana kuwa,watoto wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 14 wanaweza kukabiliwa na mashtaka ya jinai iwapo watafanya makosa ya uhalifu kwa makusudi kama vile mauaji, ubakaji au kumsababishia mtu ulemavu kwa njia ya kikatili.

Mtoto ni nani?

Mtoto katika sura ya Kidunia na Tanzania ni mtu yeyote mwenye umri wa chini ya miaka kumi na nane (18). Tafsiri hii imetokana na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, Mkataba wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto, Sera ya Maendeleo ya Mtoto na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009. 

Katika umri huu mtoto anahitaji malezi bora ili aweze kuishi vizuri, kushirikishwa, kulindwa na kuendelezwa kiakili kwa ajili ya maisha yake ya baadae ya utu uzima.

Kwa msingi huo, watoto wana haki za kipekee kwa sababu umri wao mdogo na hali ya utegemezi vinaweza kuwafanya wadhulumiwe na kutendewa vitendo vibaya. 

Watoto wote wana haki sawa bila kujali jinsia, rangi, kabila, dini, hadhi au hali ya afya. Umoja wa mataifa, Serikali, wazazi/walezi na jamii kwa ujumla wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanapatiwa haki zao. 

Kutokana na uamuzi huo wa China, huenda wameamua kukiuka makubaliano ya Kimataifa juu ya mtoto, pengine ni suala la muda, tuwape nafasi wanaweza kufanya lolote ili kurejea ustawi bora wa watoto na kuwaondolea aina hii ya vikwazo vya kisheria.

Post a Comment

0 Comments