CEO wa Simba SC Barbara afunguka mengi ikiwemo kuhusu Kichuya

Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Simba,CEO Barbara Gonzalez amesema, suala la Shiza Kichuya limesitishwa kwa kuwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) walijua kwamba wanawasiliana na mtu ambaye hayupo ndani ya Simba SC, anaripoti Mwandishi Diramakini.

CEO Gonzalez anayabainisha haya leo Desemba 21, 2020 ikiwa hivi karibuni habari zilieleza kwamba nyota huyo wa zamani wa Simba SC amefungiwa kucheza kwa muda wa miezi sita kutokana na kukiuka masuala ya usajili wake na Wekundu hao wa Msimbazi kwenye dirisha dogo la mwezi Januari.

Shiza Kichuya ambaye alirejea ndani ya Simba SC akitokea Klabu ya Pharco ya Misri ambao inaelezwa kuwa waliishtaki Simba SC kwa kumsajili mchezaji akiwa bado na mkataba jambo ambalo liliwafanya FIFA kumwadhibu huyo huku Simba ikitakiwa kulipa faini ndani ya siku 45.
“Suala la Kichuya, FIFA wanatutendea haki. Tuliwaandikia na kuwaambia hatukushirikishwa lolote na kulikuwa na mtu anawasiliana na FIFA nje ya klabu, sasa tunasubiri barua ya FIFA kwa maana ya mashitaka na wametuandikia barua kuwa tuendelee na shughuli zetu, Shiza ni mchezaji huru na Simba inaweza kuendelea kusajili.

“FIFA nao waligundua waliyekuwa wanawasiliana naye si mtendaji wala kiongozi wa Simba na Kichuya unaona anaendelea hadi hapo tutakapopokea barua kutokea FIFA,”amefafanua CEO huyo.

Wakati huo huo, Simba SC imepiga kambi kwenye hoteli ya nyota tatu ya Cresta Lodge jijini Harare Zimbabwe kujiandaa na mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushinda ile ya awali dhidi ya Plateau United ya Nigeria.

Simba SC itaikabili FC Platinum Desemba 23, 2020 ikiwa na rekodi nzuri katika mechi tano za mwisho kulinganisha na wapinzani wao, ambao wamefungwa mbili na kushinda mbili, huku ikitoka sare ya 1-1 na Al Ahly nyumbani kwa sasa. 
 
Awali CEO ameeleza kuwa, wapo tayari kwa ajili ya mchezo wao huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platinum.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili kutokana na umuhimu wake huku Simba ikiweka wazi kwamba imejipanga kupata matokeo bora.
 
Gonzalez amesema kuwa, maandalizi ambayo wameyafanya yanawapa matumaini ya kuweza kupata matokeo ambayo wanayafikiria.

"Kikosi kipo imara na maandalizi yanakwenda vizuri huku na tunaamini kwamba kwa namna ambavyo tumejipanga tuna nafasi ya kupata matokeo. Kikubwa mashabiki wazidi kutuombea na kutupa sapoti ili tuweze kushinda mchezo wetu, benchi la ufundi linatambua kwamba mchezo utakuwa mgumu na wenye ushindani ila tupo tayari,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news