Simba SC yaichapa Polisi Tanzania 2-0

Simba SC usiku wa leo wameiadhibu Polisi Tanzania ya Kilimanjaro kwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Chini ya kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck kutokana na ushindi wa leo inafikisha alama 26 baada ya kucheza mechi 12, ingawa inabaki nafasi ya tatu sasa ikizidiwa alama moja na Azam FC.  Kwani kwa sasa Azam FC imeshacheza mechi 14 ambapo Yanga SC ndio wanaoongoza Msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kw alama 34. 

Mechi ya leo imechezezwa na Refa Ahmed Aragija aliyekuwa anasaidiwa na Leonard Mkumbo wote kutoka mkoani Manyara na Martin Mwalyaje wa Tabora.

Simba SC katika mtanange ho walilazimika kusubiri hadi dakika 30 za mwisho kupata alama hizo tatu baada ya Clatous Chotta Chama kufungamabao yote hayo mawili.

Na Chama, mchezaji wa zamani wa Nchanga Rangers, ZESCO United, Lusaka Dynamos za kwao Zambia na Al Ittihad ya Misri alifunga mabao hayo baada ya kutokea benchi dakika ya 62 akichukua nafasi ya winga Mghana, Bernard Morrison.

Alifunga bao la kwanza dakika ya 63 akimalizia pasi ya mtokea benchi mwenzake, Nahodha wa timu, mshambuliaji John Raphael Bocco na bao la pili alilipachika dakika ya 89 akimalizia pasi ya kiungo mwenzake, Said Hamisi Ndemla.

Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, wenyeji Namungo FC walilazimishwa sare ya bila kufungana na Biashara United ya Mara Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Post a Comment

0 Comments