Lukuvi aagiza chuo kitafute gharama halisi urasimishaji makazi

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amemuagiza Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Huruma Lugala kukokotoa gharama halisi za uendeshaji zoezi la urasimishaji ili aweze kupanga bei ya urasimishaji anayopaswa kulipa kila wananchi,anaripoti Munir Shemweta (WANMM) Arusha.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipata maelezo kutoka kwa Mpima wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Justine Nyemele alipokwenda kukagua shughuli za Urasimishaji katika Mtaa wa Muriet jijini Arusha Desemba 21, 2020.

Lukuvi ametoa agizo hilo Desemba 21 jijini Arusha alipokwenda katika mtaa wa Muriet kukagua zoezi la urasimishaji makazi linalofanywa na chuo cha ardhi Morogoro (ARIMO).

Amesema, wakati chuo hicho cha Ardhi Morogoro kikiendesha zoezi la urasimishaji kwenye mitaa ya Mlimani, FFU, Msasani na Muriet jijini Arusha ni vyema chuo hicho kikatumia zoezi hilo kama shamba darasa kwa kukokotoa gharama halisi ili kujua kiwango anachopaswa kuchangia mwananchi kwa kuwa makampuni binafsi hayawezi kuweka viwango halisi.

"Hii mitaa minne mliyopewa kurasimisha mfanye ukokotoaji wa uhakika kujua gharama halisi ili baada ya mwisho wa mwezi Januari mtakapokamilisha kazi hiyo nitangaze viwango halisi na mkisema gharama ni 50,000 nitatangaza kiwango hicho,"amesema Lukuvi.

Kwa sasa kiwango cha mwisho kilichotangazwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ambacho mwananchi anayerasimishiwa eneo lake ni 150,000.

Kwa mujibu wa Lukuvi, awali kila kampuni ilijiwekea kiwango chake na yeye baada ya kuona viwango holela na kufikia hadi shilingi laki nne aliamua kushusha hadi 150,000 na kubainisha kuwa hakuna kampuni iliyolalamikia ushushaji kiwango hicho na kusisitiza akipata kiwango halisi atajua gharama ya kumrasimishia mwananchi kwa nyumba moja.

Amewahakikishia wananchi wa Muriet kuwa, baada ya kukamilika zoezi la urasimishaji sasa wametoka kwenye makazi holela na kuingia makazi rasmi ingawa awali wananchi hao walivunja sheria kwa kujenga kiholela na ndiyo maana serikali imewaomba kuchangia gharama za kurasimishiwa na kuwataka kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kutimiza wajibu wa kuingia kwenye makazi rasmi.


Amesema, baada ya kurasimishiwa makazi na maeneo yao kupangwa kutakuwa na faida kubwa ikiwemo upatikanaji miundo mbinu na huduma nyingine za jamii na kazi hii itasimamiwa na Mkurugenzi wa halmashauri na kuongeza kuwa wajibu wa wananchi katika kata ya Muriet ni kuchangia 150,000 ili amilikishwe.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiangalia Mawe ya Mipaka (Vigingi) vilivyojengwa na Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kwa ajili ya zoezi la Urasimishaji katika Mtaa wa Muriet jijini Arusha alipokwenda kukagua zoezi hilo Desemba 21, 2020

Amebainisha kwa kusema kuwa, wakifanya urasimishaji wanakuwa na mitaji iliyo hai na siyo mfu kama ambavyo ipo kabla ya urasimishaji na kueleza kuwa hati ya umiliki ardhi itawawezesha wananchi kuwa na usalama wa miliki wa ardhi na aliwataka watendaji wa jiji la Arusha kupita kwenye mitaa kuwahamsisha wananchi kurasimisha maeneo yao.

Lukuvi amesema, ni vigumu wananchi kuchangia kwa pamoja na kwa wakati mmoja na kutoa wito kwa mabenki kutafuta namna ya kushiriki zoezi hilo kwa kuwakopesha wamiliki 150,000 na kurejesha kiasi hicho wakati wa kuchukua hati ili zoezi hilo liende kwa kasi.

Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro, Huruma Lugala amemueleza Waziri Lukuvi kuwa, chuo chake kilianza zoezi la urasimishaji katika mtaa wa Muriet Juni mwaka huu na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo mwishoni mwa mwezi Januari 2021 kabla ya kuendelea na mitaa mingine.

Kwa mujibu wa Lugala, katika kuhakikisha kazi hiyo inakamilika haraka na kwa wakati wameamua kutumia wanafunzi wa chuo cha Ardhi Morogoro sambamba na kufyatua mawe ya mipaka ( vigingi) wenyewe ambapo kwa siku chuo chake kinafyatua vigingi 160 na kuahidi kuendelea kuongeza idadi na kufikia 200 kwa siku.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Kimanta alitumia fursa kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali kuwasamehe wananchi waliojenga kiholela ambapo baada ya zoezi la urasimishaji sasa watatambulika.

Sambamba na hilo Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameishukuru Wizara ya Ardhi kwa kuanzisha Ofisi ya Ardhi ya mkoa na kueleza kuwa uanzishwaji ofisi hiyo umeongeza uwekezaji katika huduma nzima za ardhi na kusisitiza kuwa ataendelea kuiunga mkono ofisi hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news