Mila na tamaduni Kiteto zaathiri ujasiriamali

Baadhi ya mila na tamaduni wilayani Kiteto mkoani Manyara zimetajwa kuathiri shughuli za ujasiriamali unaofanywa na jamii kukabiliana na umaskini wa kipato,anaripoti Mohamed Hamad (Diramakini) Kiteto.

Hayo yameelezwa kwenye mafunzo maalumu ya vikundi vya vikoba yanayoendeshwa na Tanzania Redcross Society kukabiliana na umaskini wa kipato katika eneo la mradi vijiji vya Olpopong, Ndaleta, Ndedo na Makame.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya vikoba yanayoendeshwa na Tanzamia Redcross Society kwa wanachama wa vikundi 10 vyenye idadi ya watu 300 wilayani Kiteto mkoani Manyara. (Picha na Mohamed Shaban/Diramakini).

Akieleza mtazamo wa jamii ya kifugaji ya Wamasai kuhusu ujasiriamali, Olendimama Ole Ngudi amesema wanaume wa kimasai hawako tayari kuruhusu wake zao kujiunga kwenye vikundi wakiamini wakipata fedha watabadilika na kuwadharau.

“Wanaume wa kimasai tunaamini wanawake wakiwa na kipato kizuri cha fedha, watatudharau kwenye familia zetu…hivyo hatuoni sababu ya kuwaruhusu ili kulinda ndoa zetu,"amedema Olendimama.

Ili tuwe salama lazima wabaki nyumbani wakiendelea kufanya kazi ndogondogo kama vile ujenzi wa nyumba, kuhakikisha watoto wanakula pamoja na kuwezesha mambo mengine kuendelea.

Amesema, kufuatia elimu inayotolewa na Tanzania Redcross Society kuhusiana na masuala ya vikoba inaweza kubadilisha mtizamo wa jamii ya kifugaji ambao mwanamke akishiriki shughuli za kiuchumi ataweza kuchangia maendeleo ya familia.

Naye mama Eliamani Julius mwanakikundi amesema pamoja na wanawake wa jamii ya kifugaji maasai kujiunga na vikundi baadhi yao wananyang’anywa fedha wanapopata na wanaume kwa madai hawapaswi kuwa nazo.

Kuna kesi nyingi kwenye ofisi za vijiji na kata na hata mahakamani kuhusu wanawake kunyang’anywa fedha na wanaume zao baada ya kuvunjwa vikoba vyao kutokana na mila na damaduni potofu mbazo zilizoshamiri kwa wamasai.

Mkufunzi wa mafunzo ya vikoba, Daniel Mollel katika mafunzo hayo Kijiji cha Ndaleta ameeleza kuwa, wengi wamenufaika nayo kwa kubadilisha maisha na kujikuta wakisomesha watoto, kujenga nyumba pamoja na kuwa na rasilimali katika familia.

Meneja wa mradi wa usalama wa chakula Kiteto, Haruni Mvungi akizungumzia mafunzo hayo amesema, jumla ya vikundi 10 vyenye idadi ya wanachama 300 wilayani Kiteto wanaendelea na mafunzo kukabiliana na umasiki wa kipato

Mkufunzi mkuu wa vikoba ofisi ya maendeleo ya jamii Kiteto, Evaline Mbwilo amesema Serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali wamefanikisha jamii kunufaika na masuala ya ujasiriamali ambapo sasa wanaendelea kubadilisha maisha yao.

Post a Comment

0 Comments