Rais Mwinyi amteua Maalim Seif kuwa Makamu wa Rais

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhe: Dkt. Hussein Ali Mwimyi amemteua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, uteuzi huo umeanza leo Desemba 6, 2020.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kwamba ,kwa kuzingatia matakwa ya Kifungu cha 9(3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachosema kwamba “Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia”.

Hatua hiyo imekuja baada ya Chama cha upinzani cha ACT Wazalendo kuafikia uamuzi wa kujiunga na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itakayokuwa na Muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Katibu Mkuu wa chama hicho cha ACT Wazalendo Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema kuwa, katika mkutano maalum wa Kamati Kuu ya chama hicho wameamua kupendekeza jina la mwanachama atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Sambamba na hayo, chama hicho pia, kimeruhusu Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge, na Madiwani waliochaguliwa kukiwakilisha chama hicho na wananchi waliowachangua kushiriki kikamilifu katika nafasi zao walizochaguliwa.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania wamemueleza Mwandishi Diramakini kuwa, uteuzi huo umefanyika ikiwa ni takwa la kisheria ambalo limetolewa na Katiba ya Zanzibar, ambayo inatamka kuwa nafasi hiyo itachukuliwa na chama ambacho kimefikisha zaidi ya asilimia 10 baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020 Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilimtangaza Dkt. Hussein Mwinyi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Rais wa Zanzibar baada ya kupata ushindi wa kura 380,402 sawa na asilimia 76.2 akifuatiwa na Maalim Seif Sharif Hamad wa Chama cha ACT Wazalendo aliyepata kura 96,103 sawa na asilimia 19.87.

Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Hamid Mahamoud Hamid alisema kuwa, wagombea urais walikuwa 17 na waliopiga kura 498,786 sawa na asilimia 88.07 ya wapiga kura 566,352 waliojiandikisha.Jaji Hamid alisema kura zilizoharibika zilikuwa 10,944 sawa na asilimia 2.19.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news