Rais Dkt.Mwinyi atoa msimamo kuhusiana na maendeleo ya Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba katika maendeleo ya watu hatokuwa na muhali (huruma) kwani muhali ndio unaoiathiri Zanzibar, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini (Pemba).

Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameyasema hayo Desemba 17, 2020 huko katika ukumbi Fidel-Castro, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba wakati alipokuwa akitoa shukukrani kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake pamoja na wazee na mabalozi wa chama hicho.

Amewaomba viongozi hao wa CCM pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kumvumilia ili achukue maamuzi magumu ili fedha za umma ziweze kuheshimiwa. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Maryam Mwinyi wakisalimiana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba, Yussuf Ali Juma alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Karume Chakechake Pemba akiwa katika ziara ya Siku mbili kisiwani Pemba, akitokea mkoani Dodoma.

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kwamba katika uongozi wake wa Urais ndani ya mwezi mmoja na nusu tu tayari amegundua kuwepo kwa ufisadi mkubwa jambo ambalo ameahidi kulifanyia kazi.

Amewaeleza viongozi hao kwamba katika uongozi wake fedha atakazozitafuta hatakubali kuchezewa hata kidogo kwani amegombea nafasi hiyo ya Urais kwa lengo la kuwatumikia wananchi.

Ameeleza dhima aliyokuwa nayo kwa Mwenyezi Mungu na kwa wananchi kwa kutekeleza aliyowaahidi na kuwataka viongozi hao kuwa tayari kwa yale yote watakayoyasikia katika kipindi hiki.

Pia ameeleza kuwa katika kipindi hiki cha kwanza katika uongozi wake lazima afanye maamuzi magumu na wala hana lengo la kutafuta mchawi na wala kufufua makaburi. 

Aidha, ameeleza kwamba katika miradi yote mikubwa iliyotekelezwa ukiwemo ule wa maendeleo ya Miji (ZUSP) ambao umegharibu Dola za Kimarekani milioni 93, miradi ya maji na miradi mengine ambayo imetumia fedha nyingi lakini matokeo yake hayaridhishi hivyo ni lazima hatua zichukuliwe juu ya ukweli wa fedha hizo.

Ameahidi kuisimamia miradi hiyo ili kuweza kupata thamani ya matumizi ya fedha zilizotumika ambazo ni nyingi na kueleza kwamba katika hatua hiyo wapo watu watakaoguswa.

Amewaeleza viongozi hao pamoja na wananchi kwamba zile ahadi alizoziahidi katika kipindi cha Kampeni za uchaguzi zitatekelezwa kwa ustadi mkubwa. 

Alisema kuwa CCM mara hii imefanya kampeni ya kisayansi ambayo ni ya aina yake na kupelekea kupata ushindi wa kishindo.

Amewapongeza viongozi wote wa CCM kisiwani humo kwa ushindi wa kishindo uliopatikana na chama hicho kutokana na kazikubwa iliyofanywa na viongozi hao, wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi.Alisisitiza kuwa rikodi iliyovunjwa ya ushindi wa kishindo uliopatikana mwaka huu hakika itavunjwa katika uchaguzi ujao waa mwaka 2025 kutokana na utendaji wa kasi utakaotekelezwa chini ya uongozi wake. 

Rais Dkt. Hussein Mwinyi amewapongeza viongozi wa dini zote kwa kuhubiri Amani wakati wote wa uchaguzi na kupelekea zoezi hilo kwenda vizuri na kuleta mafanikio makubwa.Alieleza kuwa maendeleo ya nchi yoyote hayawezi kuaptikana kama amani haipo na kueleza kuwa baada ya uchaguzi Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeundwa kwa lengo la kuleta umoja hasa katika kuleta maendeleo kwani kuwepo kwa maendeleo ni lazima watu wote waungane na kuwa wamoja.

Ameeleza kuwa, wakati umefika wa kujenga nchi na kuwataka wanaCCM kukubaliana kuwa kitu kimoja na kuondokana na malumbano ya kisiasa na badala yake kuendelea na kazi moja tu ya kuiletea nchi maendeleo. 

Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameeleza kuwa vitabu vyote vya dini vilivyoteremshwa na Mwenyezi Mungu vimeelezea umoja, hivyo kuna kila sababu ya kuhimiza umoja mingoni mwa wananachi.

Ameeleza kuwa, kuwepo kwa amani kutapelekea wepesi katika kuleta maendeleo na ndio maana wakati wa uchaguzi katika kampeni zake alizozifanya Unguja na Pemba alihubiri amani.

Amesisitiza kwamba, kazi kubwa iliyobaki hivi sasa ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2020-2025 sambamba na ahadi zote alizoziahidi wakati wa kampeni za uchaguzi.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza dhamira yake ya kutekeleza ahadi zote alizoziahidi kwa wananchi. 

Katika hotuba yake hiyo kwa viongozi hao wa CCM, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa ameunda Serikali ili kuhakikisha wale wote aliowateua wanatekeleza vyema majukumu yao.Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi aliwataka viongozi wa CCM kuendelea kuendelea kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwani bado wanadhima ya kumsaidia na kusimamia yale yote anayoyatekeleza.

Pia ametumia fursa hiyo kuwataka waandishi wa habari kwenda vijijini kutafuta changamoto za wananchi huku akieleza kuwa Wabunge, Wawakilishi, madiwani, Mashea na viongozi wengine nao pia wanadhima ya kufanya hivyo ili kuwatumikia wananchi. 

Ameeleza azma ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa sehemu maalum ya uwekezaji huku akiwaleleza viongozi haokwamba lengo ni kuhakikisha maendeleo yote yanayopatikana Unguja ni vyema yakapatikana na Pemba.Alisisitiza kwamba hatua hiyo ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa sehemu ya uwekezaji pia, itasaidia katika kupata ajira kwani yajayo yanafurahisha. 

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdallah Juma Mabodi akimkaribisha Rais Dkt. Hussein Mwinyi katika mkutano huo amewapongeza viongozi hao wa CCM kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuhakikisha wanakipa ushindi wa kishindo chama chao cha CCM kisiwani humo. 

Mapema wakitoa salamu zao viongozi hao walimpongeza Rais Dkt.Hussein Mwinyi kwa kuwajali na kuwathamini kutokana na ziara yake hiyo ya kwenda kuwapa shukurani na kuwapongeza kwa ushindi mkubwa wa chama chao kiswani humo.Viongozi hao walieleza kuwa ushindi uliopatikana mwaka huu katika uchaguzi mkuu ni wa kihistoria hasa katika Mkoa wao wa Kusini Pemba ambapo CCM imepata ushindi wa Wadi zote 19, Wabunge Majimbo 9 Uwakilishi na Ubunge Majimbo 7 pamoja na kupata nafasi neyngine zikiwemo za viti maalum. 

Walipongeza hotuba yake ya Baraza la Wawakilishi, hotuba aliyoitoa siku aliyowapisha Mawaziri pamoja na ile hotuba aloyoitoa siku ya kuwapisha Wakuu wa Mikoa.Alipongea ushindi alioupata wa asilimia 79.27 ambao tokea kuanza wka mfumo wa vyama vingi haujawahi kupatikana kisiwani humo.Rais Dk. Hussein Mwinyi alipata mapokezi makubwa kutoka kwa viongozi pamoja na wana CCM wa kisiwani Pemba mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Pemba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news