Rais Dkt.Mwinyi:Tutashirikiana na UNICEF kusimamia haki za watoto

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameliahidi Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto Duniani (UNICEF) kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendeleza ushirikiano na shirika hilo ili kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF nchini Tanzania, Bi.Shalini Bahuguna alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo pamoja na kusalimiana na Mhe.Rais leo Desemba 2, 2020. Kushoto ni Maha Damaj ambaye ni Mkuu wa Ofisi za UNICEF Zanzibar. (Picha na Ikulu/Diramakini).

Ameyasema hayo leo Desemba 2, 200 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF nchini Tanzania, Shalini Bahuguna ambapo mbali ya mazungumzo hayo Mwakilishi huyo alifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika maelezo yake Rais Dkt. Hussein Mwinyi ametumia fursa hiyo kwa kulipongeza na kulishukuru Shirika la UNICEF kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha malengo ya shirika hilo yanafikiwa hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha ustawi wa watoto kwa kusaidia huduma mbalimbali zikiwemo zile za kijamii.

Rais Dkt. Hussein amesema kwamba, Serikali ya Awamu ya Nane iko tayari kushirikiana na shirika hilo katika maeneo ya kipaumbele yaliyowekwa katika kuhakikisha mafanikio yanafikiwa.

Aidha, Rais Dkt. Hussein ametumia fursa hiyo kulipongeza shirika hilo kwa kuendelea kusaidia uimarishaji wa huduma za kijamii hapa Zanzibar hatua ambayo imekuwa ikiwasaidia watoto, vijana na hata wanawake.

Ameongeza kuwa, ushirikiano uliopo katika sekta ya afya kati ya Serikali na shirika hilo ndio yameweza kuleta mafanikio ya kupunguza vifo vya kina mama na watoto hapa Zanzibar.

Pia, Rais Dkt. Mwinyi amemuahidi Mwakilishi huyo wa UNICEF nchini kwamba changamoto zinazowakabili watoto likiwemo suala la ajira kwa watoto, ustawi wa watoto wa kiume katika sekta ya elimu vyote hivyo vinafanyiwa kazi.

Rais Dkt. Hussein ameeleza kuvutiwa na mikakati pamoja na programu mbalimbali zilizowekwa na shirika hilo hapa nchini katika kuhakikisha linaendelea kuwasaidia watoto katika nyanja mbalimbali zikiwemo huduma za elimu, afya na uwezeshaji.

Nae Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto duniani (UNICEF) nchini Tanzania, Shalini Bahuguna ameanza mazungumzo yake kwa kumpongeza Rais Dkt. Hussein kwa kuchaguliwa kwa kishindo na wananchi wa Zanzibar na kuwa Rais wao huku akiahidi kuwa shirika hilo litaendelea kumuunga mkono yeye na Serikali anayoiongoza ya Awamu ya Nane.

Mwakilishi huyo ameeleza kuwa, Shirika la UNICEF lina hitoria ya muda mrefu katika kushirikiana na kuiunga mkono Zanzibar katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuwasaidia watoto.

Ameongeza kuwa, tayari shirika hilo limeshaweka mikakati pamoja na programu mbalimbali katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi na kuondosha changamoto kadhaa zinazowakabili.

Ameeleza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua jitihada kubwa katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi na kuahidi kwamba shirika lake litaendelea kuunga mkono jitihada hizo.

Mwakilishi huyo pia, amepongeza hatua zilizochukuliwa na uongozi katika kukabiliana na kupambana na janga la COVID 19 ambapo Tanzania ikiwemo Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika kukabiliana nalo.

Kiongozi huyo ameeleza kwamba, lengo la shirika hilo ni kuhakikisha Zanzibar inapata mafanikio makubwa katika sekta ya afya hasa kwa upande wa watoto.

Sambamba na hayo, Mwakilishi huyo alipongeza juhudi za Serikali zilizofikiwa katika kupiga hatua za kupambana na vifo vya akina mama na watoto na kuweza kupunguza idadi kubwa ya akina mama na watoto wanaofariki wakati wa kujifungua.

Ameeleza kwamba, miongoni mwa mikakati iliyowekwa na shirika hilo ni kuhakikisha huduma za afya zinaongezeka ikiwa ni pamoja na kuongeza vifaa katika hospitali mbalimbali hapa Zanzibar sambamba na kuweka ustawi katika sekta ya elimu.

Ameeleza azma ya shirika hilo ya kuziendeleza programu ziliopo na kuziongeza zaidi kwa lengo la kupata mafanikio zaidi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi zikiwemo huduma zote za kijamii.

Kwa upande wake, Maha Damaj ambaye ni Mkuu wa Ofisi za UNICEF Zanzibar alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na shirika hilo katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa ushirikiano wa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane.

Post a Comment

0 Comments