Serengeti Music Festival kuwa tamasha la kwanza la kihistoria Tanzania

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amesema tarehe 26 Desemba, 2020 Dunia nzima inajua kutakuwa Tamasha la Serengeti Music Festival ambalo litakuwa mubashara (live) kuptia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii kutoka Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam,anaripoti Eleuteri Mangi, (WHUSM) Dar es Salaam.
Dkt. Abbasi amesema hayo leo Desema 25, 2020 katika kipindi maalumu cha Kibarazani kinachorushwa na kituo cha redio cha Magic Fm 92.9 cha jijini Dar es salaam ambapo aliaandamana na wasanii Mrisho Mpoto, Sister P na Shilole ili kuelezea tamasha la Serengeti. 

“Mpaka jana jioni zaidi ya wasanii 60 wamethibitisha watakuwepo kwenye tamasha na msanii wa mwisho kupanda jukwaani anatarajiwa siku ya Jumapili saa 1:45 lengo letu ni kuleta furaha kwa wananchi katika msimu huu wa mwisho wa mwaka” alisema Dkt. Abbasi. 

Dkt. Abbasi amesma kuwa Wizara ilianza kazi mara moja baada ya Serikali kuundwa na kufanyakazi ambapo tayari amekaa na wasanii, MC, DJ’s producers ili kupata maoni yao namna wanavyotafsiri maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu kuenddleza sanaa nchini. 

Matokeo ya vikao hivyo yanadhihirisha kuwa sanaa inakwenda kuwa na thamani kupitia wasanii wanajiheshimu na watasaidia kutangaza utalii wa nchi yetu hatua itakayosaidia kukuza vipato vyao na taifa kwa ujumla. 

Zaidi ya hayo, Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali imerudisha tuzo kwa wasanii katika nyanja zote ambapo zinatarajiwa kutolewa mwezi Machi 2021 ili kuwatuza waliofanya vizuri 2020 katika sekta za Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo. Hivyo, amewahimiza wadau wote wa sekta hizo kukaa mkao wa kula kwani itaandaliwa kamati ya kuratibu suala hilo na vitawekwa vigezo na masharti ili kuwa na uwazi na ukweli kwenye utoaji wa tuzo hizo. 

Aidha, Dkt. Abbasi amewasisitiza wasanii kumuenzi Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza kwa kufanya muziki wenye heshima na adabu unaozingatia maadili ya kitanzania kwani Bw. Godfrey Mngereza alikuwa akiwasisitiza wasanii kuzingatia maadili kwenye nyimbo zao wakati wa uhai wake. 

Kwa upande wake Msanii Shilole ambaye ni mmoja wa wasanii watakaotumbuiza kwenye jukwaa wakati wa tamasha la Serengeti Music Festival ameahidi kufanya show ya kufa na kupona ili mashabiki watakaofika uwanja wa Uhuru wapate burudani ya aina yake ambapo ataimba nyimbo zake zote kuanzia Igunga mpaka wimbo wake mpya wa “My Photographer”. Huku msanii Mrisho Mpoto maarufu kama Mjomba akisisitiza kuwa shughuli ya kesho ni moja tu watu waje kushuhudia dunia inavyosimama kupitia Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam. 

Wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya (Bongo Fleva) wa sasa na wa zamani watakuwepo kwenye tamasha hilo ambalo litajumuisha pia wanamuziki wa nyimbo za Injili, Singeli, Sanaa za Maonesho ikiwemo Maigizo ya Jukwaani, Sarakasi na pamoja na Filamu fupi za Bongo Movie zitaoneshwa. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news