UNHCR lapinga wakimbizi kuhamishiwa katika kisiwa hatari

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema linapinga kuhamishwa kwa wakimbizi wa Rohingya kutoka Cox Bazar, Bangladesh,kwenda kisiwa cha mbali katika Ghuba ya Bengal, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Wakimbizi wakiwa katika kambi kubwa ya Cox Bazar. (Picha na nrc)
Mamlaka nchini Bangladeshi mwishoni mwa wiki ilihamisha zaidi ya wakimbizi 1,500 wa Rohingya kwenda Bhasan Char, ghuba isiyo na wakazi ya kisiwa cha Bengal ambayo inatajwa inaweza kuathiriwa na vimbunga na kukabiliwa na mafuriko makubwa.

Msemaji Mkuu wa Ofisi ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa, Babar Baloch amesema Umoja wa Mataifa haukuhusika katika kuandaa harakati hiyo.

Baloch amesema, hakujua ni wakimbizi gani na hakuwa na habari za kina juu ya operesheni ya jumla ya uhamishaji huo.

Anasema, UNHCR ina wasiwasi kuwa wakimbizi wa Rohingya hawakuwa na taarifa waliyohitaji kufanya uamuzi huru na ulio na taarifa kamili juu ya kuhamia Bhasan Char.

“Tumesikia ripoti kutoka kwenye kambi kwamba baadhi ya wakimbizi wanaweza kuhisi wanashinikizwa kuhamia Bhasan Char au labda wamebadilisha maoni yao ya mwanzo juu ya kuhamishwa na hawataki tena kuhama. Ikiwa ni hivyo, wanapaswa kuruhusiwa kubaki katika kambi hizo,”amesema Baloch.

Mwaka 2017, karibu wakimbizi milioni moja walitoroka mateso na vurugu huko Myanmar na kwenda Cox's Bazar ambako wanaishi katika kambi duni zenye msongamano wa watu.

Serikali ya Bangladesh inasema inataka kupunguza msongamano katika kambi hizo na inaona kuwahamisha hivi karibuni wakimbizi hao ni hatua ya kwanza katika mpango wa kuhamisha wakimbizi 100,000 kwenda Bhasan Char.

Post a Comment

0 Comments