Wafanyabiashara waishika mkono Mlandege FC, Rais Dkt.Mwinyi aagiza

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha Vyama vya Michezo vinakuwa na utaratibu maalum utakaowezesha wafanyabiashara kujitokeza na kudhamini michezo hiyo, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimkabidhi fedha tasilimu za Kitanzania milioni 35 Mwenyekiti wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Mlandege, Ali Khatib Dai,ambapo timu hiyo inatarajiwa kusafiri kwenda mjini Tunis,Tunisia katika mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika ambapo wanakwenda kukabiliana na timu ya CS SFAXIEN ya Tunisia.

Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Desemba 2, 2020 Ikulu jijini Zanzibar katika hafla ya makabidhiano ya fedha zilizotolewa na wafanyabiashara watano wa Zanzibar kwa ajili ya ushiriki wa Timu ya Mlandege, kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Timu ya CS Sfaxien ya Tunisia.

Amesema, maendeleo ya michezo hapa nchini yatafikiwa kwa kuwepo udhamini wa uhakika utakaozinufaisha pande zote mbili kati ya wafanyabaishara na vilabu.

Amewataka wafanyabiashara kote nchini kujitokeza kusaidia maendeleeo ya michezo, ikiwemo soka ili kurejesha hadhi ya mchezo huo iliyopotea.

Rais amesema kwa njia yoyote ile Taifa lina dhima ya kuhakikisha michezo inaimarika na kubainisha kuwa kamwe jambo hilo haliwezi kufikiwa bila ya kuwepo ufadhili ambapo makampuni kwa utaratibu maalum yataweka fedha katika bajeti zao.

Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa wizara hiyo kusimamia mashindnao mbalimbali, akisema jambo hilo lina faida kubwa katika maendeleo ya michezo, kwa kigezo kuwa huongeza hamasa, kuinua kipato pamoja na kukuza utalii nchini.

Aidha, ameitaka wizara hiyo kuendelea na juhudi za kutengeneza viwanja kila mahali, ili kuondokana na utaratibu wa timu kupokezana viwanja.

Dkt.Mwinyi amesisitiza azma ya vyama vya michezo kukaa na wadau, ili kujenga ushirikiano na maelewano kati ya vyama vya michezo na vilabu pamoja na wadau kwa ujumla.

Amesema hivi sasa maelewano kati ya viongozi wa ZFF na vilabu Unguja na Pemba hayako sawa, sambamba na kuwepo tatizo kubwa la ukosefu wa fedha za kuendeshea mashindano.

Dkt.Mwinyi amewashukuru wafanyabiashara hao kutoka kampuni mbalimbali hapa Zanzibar kwa uzalendo wao wa kusaidia fedha zitakazoiwezesha timu ya Mlandege kugharamia safari ya kuelekea nchini Tunisia. "Nawashukuru kwa kuokoa hili jahazi, hili jambo mlilolifanya ni la kizalendo sana,"amesema.

Mapema, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Mwita Maulid ameahidi kukaa na wadau ili kuimarisha maendeleo ya michezo nchini pamoja na maandalizi ya kufanikisha Kombe la Mapinduzi la 2021, kwa dhamira ya kurejesha hamasa na imani kwa wananchi.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Omar Hassan Omar ‘King’ ameishukuru Serikali kwa wito wake wa kuitaka wizara hiyo kuwakutanisha na wadau wa michezo ili kufanikisha safari ya timu ya Mlendege kuelekea nchini Tunisia.

Pamoja na mambo mengine, akigusia kushuka kwa michezo nchini amesema, kwa kipindi kirefu Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na changmoto ya miundombinu ya michezo na ndio maana Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ilani yake ikaazimia umuhimu wa kujenga viwanja katika wilaya zote Unguja na Pemba.

Amesema, mfumo wa uendeshaji wa mpira wa miguu nchini nao ulighubikwa na changamoto kubwa ya kuwa na idadi kubwa ya timu zinazoshiriki katika Ligi Kuu ya Zanzibar, jambo lisiloendana na maelekezo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Amesema, kuwepo kwa timu 36 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar, hakuwezi kuwashajiisha wadhamini kuwekeza katika mpira hapa nchini.

Aidha,  King amesema kuna changamoto ya mfumo wa kiutawala katika uendeshaji wa vyama vya michezo ikiwemo ZFF ambapo katiba yake inapaswa kuwa na sifa zinazoendana na vyama vya soka vya nchi nyingine zilizo wanachama wa FIFA.

Nao wafanyabiashara waliofadhili fedha hizo wamesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwashirikisha wadau wa michezo katika kila hatua ili kufanikisha maendeleo ya michezo nchini, ikiwemo soka.

Wamesema, mchezo wa soka uliopata umaarufu mkubwa hapa nchini katika miaka iliyopita, umepoteza hadhi na hamasa kutokana an sababu mbali mbali, ikiwemo kutokuwepo ushirikishwaji wa wadau pamoja na mfumo mbaya wa uendeshaji.

Aidha, akitoa shukrani, Mkurugenzi wa Klabu ya Mlandege, Ali Khatibu Dai amewashukuru wafanyabiashara hao kwa kujitolea kufanikisha safari ya timu hiyo kuelekea nchini Tunisia katika pambano la marudiano dhidi ya timu ya CS Sfaxien.

Amesema, miongoni mwa athari kubwa ambayo Klabu ya Mlandege ingekabiliana nayo kwa kushindwa kushiriki katika mchezo huo wa marudiano ni kufungiwa na CAF, na hivyo kuliletea aibu Taifa.Jumla ya Dola za Kimarekani 34, 000 zimechangwa na wafanyabaishara hao watano kutoka Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news