Waziri Mkuu afanya ziara Hospitali ya Uhuru

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekagua umaliziaji wa ujenzi wa Hospitali ya Uhuru unaoendelea katika Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma na kuagiza huduma zianze kutolewa ifikapo Desemba 20, mwaka huu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua kazi ya umaliziaji wa ujenzi wa hospitali ya Uhuru wilayani Chamwino, Dodoma, Desemba 6, 2020. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa SUMA JKT, Brigedia Jenerali Rajabu Mabele.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amekagua hospitali hiyo leo Desemba 6, 2020 na amesema vifaa vyote zikiwemo samani, vifaa tiba vinavyotakiwa kuwepo kwenye hospitali hiyo vipelekwe na vifungwe ili huduma zianze kutolewa.

“Tunakusudia kumuomba Mheshimiwa Rais Dkt.John Pombe Magufuli aje kuzindua hospitali hii kabla ya Desemba 30, mwaka huu, hakikisheni vifaa vyote zikiwemo samani na vifaa tiba vinaletwa na kufungwa ili Desemba 20, mwaka huu huduma zianze kutolewa,”amesema Majaliwa.

Desemba 3, mwaka huu Rais Dkt.Magufuli aliahirisha maadhimisho ya sherehe za miaka 59 Uhuru zilizotarajiwa kufanyika Desemba 9, 2020 na kuelekeza kiasi cha shilingi milioni 835,498,700 zilizotengwa kwa ajili ya sherehe za hizo zitumike kununulia vifaa mbalimbali kwa ajili ya Hospitali ya Uhuru.

Mbali na ununuzi wa vifaa hivyo, pia Rais Dkt.Magufuli aliagiza fedha hizo zitumike kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa kuzunguka eneo la hospitali hiyo pamoja na ujenzi wa barabara ya kuingilia hospitalini hapo.

Hadi kufikia sasa ujenzi wa hospitali hiyo ya Uhuru umegharimu shilingi bilioni 4.2. Januari 2019 wakati akipokea gawio la hisa za kampuni ya Simu ya Airtel Rais Dkt. Magufuli aliagiza kiasi cha shilingi 2,415,151,650.00 zilizotolewa na kampuni hiyo zitumike katika ujenzi wa hospitali hiyo.

Novemba 20, 2018, Rais Dkt.Magufuli aliagiza kiasi cha sh.milioni 995,182,000.00 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru zitumike kujenga Hospitali ya Uhuru, ambayo kwa sasa ujenzi wake upo katika hatua za umaliziaji.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya 59 ya Uhuru kwa mwaka huu inasema; ‘Miaka 59 ya Uhuru na Miaka 58 ya Jamhuri: Tanzania yenye Uchumi Imara Itajengwa na Watanzania Wenyewe, Tufanye Kazi kwa Bidii, Uwajibikaji na Uadilifu.’

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge ameishukuru Serikali kwa uboreshaji wa huduma za afya mkoani Dodoma ukiwemo ujenzi wa hospitali hiyo ya Uhuru, ambapo ameiomba iwaongezee wataalamu wa afya.

Amesema, mahitaji ya wataalamu wa afya wakiwemo madaktari katika mkoa ni 2,505 huku waliopo ni wataalamu 1,767, hivyo ameomba Serikali iwasaidie kutatua changamoto hiyo kwa kuajiri wataalamu wa kutosha katika sekta hiyo.

Pia, Dkt. Mahenge amesema, Hospitali ya Benjamin Mkapa inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nyumba za wataalam, ambapo aliomba msaada wa ujenzi wa nyumba hizo ili kuwawezesha watoa huduma hao kuwa na makazi karibu na hospitali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news