Waziri Ummy ajitambulisha kwa Rais wa Zanzibar Dkt.Mwinyi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu hii leo amefanya ziara ya kikazi visiwani Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha,anaripoti Lulu Mussa.
Waziri Ummy amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi Ikulu Zanzibar. Katika mazungumzo yao Mhe. Mwalimu amesema kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais – Zanzibar amedhamiria kuendeleza jitihada za kutatua changamoto za Muungano zilizobakia.


“Mhe. Rais nikuhakikishie kuwa nitafanya kazi kwa karibu sana na
Mhe. Khalid Waziri mwenzangu kuhakikisha hoja ambazo bado hazijapatiwa
ufumbuzi zinafanyiwa kazi na mwanzoni mwa mwezi Januari tunategemea kuwa
na kikao cha pamoja baina yetu” Alisisitiza Mhe. Ummy.
Kwa
upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.
Dkt. Hussein Ali Mwinyi amempongeza Mhe. Ummy Mwalimu wa kuteuliwa tena
kuwa Waziri na kusisitiza kuwa Serikali yake itampa ushirikiano katika
kuratibu masuala ya Muungano.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy Mwalimu amefanya mazungumzo na Makamu
wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharrif Hamad Chukwani Zanzibar.
Mhe.
Hamad amesisitiza umuhimu wa Wizara zenye hoja za Muungano kukutana na
kutafuta suluhu ya mapema na kuhamasisha Wizara zisizo na hoja kukutana
pia kwa lengo la kudumisha undugu baina ya Tanzania bara na Tanzania
Zanzibar.


“Nashauri na kusisitiza Wizara zinazoshabihiana zikutane na kuhakikisha hoja zinazopatiwa ufumbuzi zitekelezwe ipasavyo” alisisitiza Maalimu Seif Sharif Hamad.
Waziri Ummy Mwalimu yuko visiwani Zanzibar kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na hapo kesho atatembelea miradi ya Muungano inayotekelezwa pande zote mbili.
No comments