Dkt.Mabula ashangazwa na halmashauri kuingia mikataba na warasimishaji bila kuwachunguza

Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula ameshangazwa na halmashauri za mkoa wa Kilimanjaro kuingia mikataba ya urasimishaji na makampuni zaidi ya nane ambayo yameshindwa kukamilisha kazi suala lililosababisha makampuni hayo kuanza kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU),anaripoti Munir Shemweta, (WANMM) Kilimanjaro.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwasili katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro kuanza ziara ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi Januari 8, 2021. 

Akizungumza na uongozi wa mkoa wa Kilimanjaro, wakurugenzi wa halmashauri, watendaji wa sekta ya ardhi na Makampuni ya urasimishaji katika kikao chake kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkoa wa Kilimanjaro Januari 8, 2021 akiwa katika ziara ya siku moja, Dkt. Mabula amesema haiwezekani wakurugenzi wote wa halmashauri kuingia mikataba na makampuni zaidi ya nane ya urasimishaji katika mkoa na yashindwe kukamilisha kazi. 

"Wakurugenzi wote mko hapa wakati mnaingia mikataba na makampuni ya urasimishaji mliwachunguza kabla ya kuingia mikataba? maana haiwezekani mkoa mzima makampuni yashindwe kukamilisha kazi kwa wakati na naagiza halmashauri zifanye uchunguzi kabla ya kuyapa kazi makampuni,”amesema Dkt. Mabula. 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati ya Ardhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Kastori Msigala wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Kilimanjaro.

Amesema, Makampuni ya upimaji hayatakiwi kwenda kinyume na mpango uliowekwa na halmashauri na yanatakiwa kufanya kazi kwa kwenda mtaa kwa mtaa na siyo mtu kwa mtu na kuongeza kuwa halmashauri zinatakiwa kuyachunguza na kuchukua makampuni yenye uwezo na mtaji na siyo kutegemea fedha za wananchi.

Ameiagiza Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji na Makampuni kuyachunguza makampuni yote ya urasimishaji ambayo hajakamilisha kazi na wakibaini kampuni zisizo kuwa na uwezo basi zifutwe kufanya kazi tena ya upangaji na upimaji nchini. 
Sehemu ya watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Kilimanjaro wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema kuwa, Wizara ya Ardhi iliona jambo jema kushirikisha sekta binafsi katika zoezi la urasimishaji kwa lengo la kuongeza kasi ya upimaji na kusisitiza kuwa Wizara ya Ardhi inachotaka ni Kampuni inayopewa kazi ni kuwa na angalau asilimia 50 ya mtaji wa kufanya kazi badala ya kutegemea fedha za wananchi. 

“Wizara inasema kama huna fedha usitegemee pesa za wananchi kuendesha kazi ya urasimishaji na tusiwafanye wananchi ndiyo mtaji kwa kuwa mwisho itakuwa kero kwa kushindwa kukamilisha kazi,”amesema Dkt.Mabula.

Mkurugenzi Mtendaji wa moja ya Kampuni za Urasimishaji katika mkoa wa Kilimanjaro ya KILI Surveys LTD, Alphonce Mwanshinga alijitetea mbele ya Naibu Waziri Dkt.Mabula kwa kueleza kuwa kampuni yake tayari imeshapima viwanja 2,795 na kulipwa shilingi milioni 283,361 huku ikiendelea kudai milioni 247,639,000 kutoka kwa wananchi. 

Hata hivyo, amesema changamoto kubwa kwa kampuni yake kushindwa kukamilisha zoezi hilo kwa wakati ni kuwa walipoanza kazi waliendesha zoezi kulingana na uitikio wa wananchi na kuamua kupima kwa wale waliolipa fedha na kuongeza kuwa kampuni yake ya KILI Surveyers LTD inatarajia kukamilisha zoezi la upimaji katika mtaa waliopewa mwisho wa mwezi Januari 2021. 

Baadhi ya Makampuni yaliyopewa kazi ya urasimishaji kwenye mkoa wa Kilimanjaro ni pamoja na Kili Surveys Ltd, Makazi Solution, EM& Contruction Ltd, Land Surveys and Consultancy Services pamoja na Kampuni ya EM Land Consultants.

Post a Comment

0 Comments