Mshikamano wa Rais Dkt.Mwinyi, Maalim Seif wazidi kupongezwa, Seif asisitiza ni mwendo wa kujenga nchi, kuwaletea wananchi maendeleo

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameendelea na siku ya pili ya ziara yake kisiwani Pemba kwa kukutana na wananchi wa Wilaya ya Micheweni na Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Awali wadau mbalimbali wameueleza mtandao huu wa Diramakini kuwa, Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kushirikiana na Maalim Seif, Makamu wa Pili wa Rais na watendaji wengine imeonyesha mwelekeo chanya ambao umewapa matumaini makubwa wananchi kuelekea katika hatua nzuri ya maendeleo.

"Tunawapongeza sana hawa viongozi wetu, jambo muhimu kwetu ni kuendelea kuwaombea na kufanya kazi kwa bidii, kupendana, kushirikiana na inshallah, Mwenyenzi Mungu atatupa baraka tele kwetu sisi na nchi yetu,"amesema Said Khamis mkazi wa mjini hapa.
Aidha, Maalim Seif ameanza kwa kukutana na wananchi wa makundi mbalimbali ambao ni viongozi wa Serikali,viongozi wa Dini,watu mashuhuri, wazee, vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum (walemavu), kutoka Wilaya ya Micheweni na baadae Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amekutana na wananchi wa Wilaya ya Micheweni katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Karume Micheweni, na baadae kumalizia Wilaya ya Wete ambapo alikutana na Wananchi wa Wilaya hio katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete.

Katika Wilaya zote mbili Makamu wa Kwanza aliendelea kuwakumbusha wananchi asili ya Zanzibar, tunu za Zanzibar, historia ya Zanzibar sambamba na kuonesha umuhimu wa kushirikiana na kuwa kitu kimoja katika jamii zao kwani Wazanzibar ni wamoja.
Katika kusisitiza jambo hilo Maalim Seif amesema;"Najua kuleta umoja muda mwengine ni kazi ngumu na inaweza kuchukua muda, lakini jambo litakalotufikisha huko ni dhamira zetu njema".

Maalim Seif amewaambia wananchi hao kwamba ni kweli yapo maumivu na madhila mengi ambayo yalishafanyika, lakini bado ipo haja ya kuyazika ya nyuma na kuyasahau, na kuongezea kwa kusema;

"Wazanzibari kama kuumia tulishaumia sana kama kuteseka tulishateseka sana kwa sasa tunasema sasa basi, tuamue kushirikiana na kujenga nchi yetu".

Kuhusu uhasama unaotokea kutokana na vyama vya siasa Maalim Seif amefafanua kwa kusema,

"Uhasama wa vyama vya siasa ulianza miaka mingi tangu enzi za Afroshiraz Party, ila hatupaswi kufukua makaburi haya, wala hatupaswi kuifuata historia mbaya na badala yake tuungane tuipeleke Zanzibar katika mustakbali mwema, Zanzibar ni yetu".

Maalim ameendelea kusisitiza kwamba ingawa Katiba inaturuhusu kila mtu awe na chama chake cha siasa, lakini uwepo wa vyama vya siasa visitutoe katika dhamira njema ya Uzanzibari wetu, kwani maslahi ya Wazanzibar ni zaidi kuliko vyama vya siasa.

Baada ya hotuba yake Makamu wa Kwanza alitoa fursa kwa wananchi wa wilaya hizo kutoa michango yao ama kuuliza swali na kuyatolea ufafanuzi.

Akiwa Wilaya ya Micheweni Maalim Seif alifika Kijiji cha Wingwi Njuguni kukagua soko la samaki la Njuguni.

Mwisho wa ziara yake Makamu wa Kwanza wa Rais ametembelea sehemu maalum ya uwekezaji wa Viwanda Chamanangwe Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Post a Comment

0 Comments