Rais Dkt. Mwinyi:Hongereni wananchi kwa kuendelea kudumisha umoja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa utayari wao wa kuendeleza umoja na kuacha mifarakano, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi (wa tatu kushoto) akisikiliza hotuba pamoja na waumini mbalimbali iliyotolewa na Sheikh Ali Fakih Abdallah wakati aliposhiriki katika sala ya Ijumaa Iliyoswaliwa leo Januari 8, 2021 katika masjid Raudhwa Darajabovu Wilaya ya Mjini Unguja. (Picha na Ikulu/ Diramakini).

Mheshimuwa Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Januari 8, 2021 huko katika Msikiti Raudha uliopo Darajabovu, Jimbo la Shauri Moyo Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akitoa salamu zake kwa Waislamu mara baada ya kukamilisha Sala ya Ijumaa 

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa, kwa upande wao wakiwa viongozi wa kisiasa tayari wameonesha nia na njia kwa kuingia katika makubailiano ya kujenga Serikali ya Umoja wa Kitaifa lengo ni kuwafanya wafuasi wao wa kiitikadi za kichama kuacha mifarakano na kuwa wamoja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akifuatana na wasaidizi wake mara baada ya sala ya Ijumaa aliposhiriki pamoja na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Masjid Raudhwa Darajabovu Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi.(Picha na Ikulu/ Diramakini).

Alhaj Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa wananchi wa Zanzibar kwa kukamilisha uchaguzi kwa salama na amani kwani ni uzoefu uliopo kwamba wakati wa uchaguzi amani hutoweka. 

Akieleza kuhusu umuhimu wa umoja, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa, kuna umuhimu wa kuwepo kwa umoja wa kitaifa kwani vitabu vyote vya dini vimesisitiza suala la umoja hasa ikizingatiwa kwamba umoja hupelekea hata mambo ya kidunia yakiwemo maendeleo kuimarika.

Amesema kuwa, amani na umoja ndio msingi wa maendeleo hivyo, kuna kila sababu ya kuidumisha kwa maslahi ya nchi na wananchi wote wa Zanzibar.
Baadhi ya waumini wa Dini ya Kiislamu waliohudhuria katika sala ya Ijumaa wakisikiliza hotuba iliyotolewa na Sheikh Ali Fakih Abdallah katika Masjid Raudhwa Darajabovu Wilaya ya Mjini Unguja ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) alishiriki nao katika sala hiyo.(Picha na Ikulu/ Diramakini).

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa, katika kampeni za uchaguzi uliopita aliomba kuwa kiongozi kwa lengo la kutaka kuwatumikia wananachi kwa kuwaletea maendeleo yao. 

Mheshimiwa Rais amesema kuwa, Serikali anayoioongoza imejipanga vyema katika kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka kutokana na kuwepo kwa amani na umoja wa kitaifa.

Ameongeza kuwa, atahakikisha juhudi za makusudi zinachukuliwa katika kutekeleza ahadi zilizoahidiwa kwa azma ya kuyafanya maisha ya Wazanzibari kuwa bora zaidi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia aliyesimama) akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu na kutoa nasaha zake mara baada ya Sala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo katika Masjid Raudhwa Darajabovu Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi.(Picha na Ikulu/ Diramakini).

Sambamba na hayo, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa, huduma zote muhimu za kijamii zilizoahidiwa zikiwemo afya, elimu, maji, barabara na nyinginezo zitatekelezwa na kuwataka wananchi kuendelea kuomba dua ili kupatikana wepesi wa kuyatekeleza. 

Alhaj Dkt. Mwinyi alilipokea ombi la Waumini wa Msikiti huo wa kutaka kumaliziwa jengo la msikiti wao na kuahidi kuwasaidia ili msikiti huo uweze kusalika vyema na waumini wote wa eneo hilo waweze kupata nafasi nzuri ya kuweza kufanya ibada zao.

Alhaj Dkt.Mwinyi aliushukuru uongozi wa msikiti huo kwa mapokezi makubwa aliyoyapata pamoja na mapenzi yao ya kutaka kusali na yeye japo kwa siku moja. 

Mapema Sheikh Ali Fakih Abdallah akitoa hotuba ya sala ya Ijumaa alieleza kwamba hatua na juhudi zilizochukuliwa na Rais Dkt. Mwinyi za kuimarisha umoja, mshikamano kwa kuleta maridhiano katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa anayoingoza ambayo imeondosha mifarakano.Alisema kuwa jambo hilo la kheri lilianza kufanywa na kiongozi wa Waislamu Mtume Muhammad (S.A.W), kwa kuyaungaisha makabila yaliyokuwa hasimu ya wakati huo Aus na Khazraj na hatimae kuwa wamoja. 

Waumini hao pia, walimpongeza Alhaj Dk. Mwinyi kwa uongozi wake bora ambao amekuwa akiwajali watu wote wakiwemo wanyonge katika kuwapigania haki zao huku Waumini hao wakitumia fursa hiyo kumuombea dua ili atekeleze vyema majukumu yake ya Urais.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news