Rais Dkt.Mwinyi:Tumepunguza shamrashamra mwaka huu kuokoa fedha za umma

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imelazimika kupunguza baadhi ya shamrashamra za maadhimisho ya kusherehekea miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuokoa fedha na kuzielekeza katika matumizi mengine ya serikali ikiwemo huduma za kijamii, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Januari 12, 2021 katika kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizofanyika jana katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini hapa.

Amesema, Serikali ilikuwa na azma ya kuzipamba sherehe hizo kwa shamrashamra mbalimbali kama ilivyozoeleka na Wazanzibari wote, lakini kutokana na hali ya uchumi, sherehe hizo zimetekelezwa kwa njia tofauti na ilivyozoeleka.
Amesema, hali ya uchumi wa Dunia imeyumba sana kutokana na madhara ya ugonjwa wa COVID 19, hivyo kuilazimu Serikali kutumia fedha za sherehe hizo katika kufidia mapengo ya wajibu kwa wananchi, ikiwemo huduma za elimu, afya na nyinginezo.

Ameeleza kuwa, hali hiyo ni ya mpito na kubainisha kawa pale itakapotengemaa (katika siku za usoni), utaratibu wa kawaida wa maadhimisho ya sherehe hizo utarejea.

Dkt.Mwinyi amesisitiza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuendelea kuyalinda Mapinduzi ya 1964 katika msukumo mpya wa kiuchumi.

Amesema, wakati umefika kwa Wazanzibari kujikita katika Uchumi wa Buluu, kwa kuzingatia shabaha ya Mapinduzi hayo ambayo ni kustawisha maisha ya wananchi wake.

Aidha, amesema Wazanzibari wanapaswa kupata huduma bora na stahili, ikiwemo elimu, afya na maji na kwa wale watakaohitaji kufanya biashara waweze kufanya shughuli zao bila kiuzuizi wala vikwazo vitokanavyo na rushwa.

Amesema, Mapinduzi ya kiuchumi ndio mapinduzi yatakayotoa majibu ya changamoto ziliopo na vizazi vijavyo. 

“Tunapaswa kuleta Mapinduzi katika sekta za Uvuvi ili wavuvi wetu wavue kwa zana za kisasa na tuweze kufaidika na rasilimali za bahari kuu, tunapaswa kuleta Mapinduzi katika kilimo ili wakulima wetu waongeze tija na kutuondolea utegemezi wa chakula kutoka nje pamoja na kuinua zao la karafuu na Mwani,”amesema.

Amesema, Wazanzibari wanahitaji Mapinduzi katika sheria na taasisi ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila bughudha wala vikwazo pamoja na kuwepo Mapinduzi katika Sanaa na Michezo ili kila mmoja aweze kutumia uwezo na kipaji chake kucheza na kujiendeleza kimaisha.

Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi alisema Mapinduzi yanayohitajika yatawezekana endapo mambo tofauti yatatekelezwa, ikiwemo kuufungua Uchumi kwa kuweka mazingira mazuri.

Amesema, ni azma ya serikali anayoiongoza kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kuendeleeza uchumi wa buluu.

“Lengo ni kufungamanisha sekta za uvuvi, utalii na uchukuzi kwa kupanua shughuli za Utalii ikiwemo uwekezaji wa Utalii kisiwani Pemba, kujenga Bandari mpya za Mangapwani na Maruhubi ili kuwawezesha wavuvi wetu kuvua kisasa zaidi ikiwemo uwekezaji wa Uvuvi wa Bahari kuu,”amesema.

Aidha, amesema eneo jingine linalohitaji Mapinduzi ni kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa kodi mbalimbali.

Alisema, hatua hiyo italiwezesha Taifa kuendelea sambamba na kumudu kupanua wigo katika utoaji wa huduma za kijamii kama vile afya, elimu na nyinginezo ikizingatiwa kuwa hivi sasa huduma hizo zinatolewa bure na serikali

Ameeleza suala la umoja wa kitaifa ni nguzo muhimu katika ujenzi wa Zanzibar mpya na kusema ndio sababu zilizomsukuma kuchukua hatua za haraka katika kujenga maridhiano ya umoja wa kitaifa. 

Amesema, hatua hiyo ni utekelezaji wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 toleo la 2010 lililobainisha haja ya kundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa hapa nchini, hivyo akawataka viongozi kufanya kazi ya kuyatafsiri
maridhiano hayo ili kuwaletea neema Wazanzibari.

Akigusia changamoto ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia unaolikabili taifa, Dkt. Mwinyi alisema jambo hilo linafedhehesha sana na kuchafua taswira ya Zanzibar.

Amesema katika kulikabili jambo hilo, kilio cha wananchi kimeelekezwa kwa vyombo vya husika kwa kushindwa kuchukua hatua pale taarifa zinapotolewa pamoja na baadhi ya wazazi na ndugu kuyamaliza masuala hayo kifamilia kwa kile kinachodaiwa kuficha aibu na kunusuru udugu.

Ametoa wito wa kukomeshwa vitendo hivyo mara moja pamoja na kuagiza kuwachukulia hatua za kisheria watu wote watakaopatikana huhusika na vitendo hivyo bila kuzingatia uhusiano uliopo ama uzawa.

Amesema, kushindwa kuwachukulia hatua wahalifu wa matukio ya udhalilishaji ni kuwasaliti watoto wa Zanzibar ambapo Serikali ina wajibu wa kuwalinda.

Rais Dkt.Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa kuhifadhi ‘Mali Kale’ , akibainisha kuwa ni urithi muhimu katika historia ya Taifa hili.

“Sote tumesikitishwa kwa tukio la kuangauka sehemu ya jengo la Kihistoria la Beit el Ajaib ambalo lilikuwa katika ukarabati, naungana na Wanzazibari wote na kutoa pole kwa ndugu na jamaa wa wananchi wawili waliopoteza maisha,”amesema.

Ameeleza kuwa, kuanguka kwa jengo hilo kunawakumbusha Wazanzibari umuhimu wa kuyakarabati mara kwa mara majengo yaliopo Mji Mkongwe ikiwa ndio alama ya Zanzibar.

Aidha, Dkt.Mwinyi amewashukuru viongozi, wapiganaji wa vikosi vya ulinzi na usalama, watumishi, waandishi wa habari na wananachi kwa kufanikisha vyema sherehe hizo pamoja na kutumia fursa hiyo kuwataka wananchi hao kuwaombea dua marehemu wote waliotoa maisha yao katika ukombozi wa taifa lao.

Mapema, Mwenyekiti wa Kamati ya sherehe ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla alisema Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 yalikuwa na lengo la kumkomboa Mzanzibari kutokana na dhuluma za kutawaliwa.

Amesema, maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, yamehusisha matukio mbalimbali ikiwemo usafi wa mazingira, ufunguzi na uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 46.1.

Aidha, amesema kulifanyika mazoezi ya viungo, Tamasha la Biashara, upigaji wa Fash-fash pamoja na kufanyika michezo mbalimbali ikiwemo Kombe la Mapinduzi.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha miradi mitatu iliowekewa mawe ya msingi inakamilika kwa ufanisi mkubwa ili kuweza kutoa huduma bora kwa jamii.

Ametoa shukurani kwa wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika sherehe hizo, sambamba na kwenye matukio ya uwekeaji mawe ya msingi, hatua aliyosema inabainisha utayari walionao katika kuendeleea kuyalinda Mapinduzi hayo.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa akiwemo Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, Rais mstaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi pamoja Marais wastaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume na Dkt. Ali Mohamed Shein.

Wengine ni viongozi wakuu wa Kitaifa kutoka Serikali ya Jamuhuri ya Muuungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wake wa viongozi wakuu wastaafu wa SMT na SMZ, Mabalozi wadogo wa nchi mbalimbali waliopo Zanzibar, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Wakuu wa Mikoa ya Zanzibar, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Mawaziri, Viongozi wa Vyama vya Siasa,Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama.
Aidha, sherehe hizo zilipambwa kwa maonyesho mbalimbali, ikiwemo maandamano yalioongozwa na Kikundi cha Bendi ya Chipukizi, Vijana wa makundi mbalimbali, wananachi kutoka mikoa mitano ya Unguja na Pemba, Skauti pamoja na vijana wa Chipukizi.

Vile vile, kuliwepo maonyesho ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama, vilivyoshirikisha JWTZ, Polisi, Uhamiaji, KMKM, Mafunzo, JKU pamoja na KVZ ambapo kwa njia tatu tofauti walitembea (root much) kutoka Kambi ya JWTZ Mtoni hadi Ziwani Polisi na hatimae kupita mbele ya mgeni rasmi na kutoa heshima, sambamba na kuwepo maonyesho ya ‘Showforce’, ambapo magari na vifaa mbalimbali vinavyotumiwa na wapiganaji hao vilipita mbele ya mgeni rasmi Dkt. Hussein Mwinyi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news