RIPOTI MAALUM: TAKUKURU Kagera inavyong'ata

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imeendelea kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, namba 11 ya mwaka 2007, anaripoti Mwandishi Diramakini. 
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera, John K.E Joseph. 

Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera, John K.E Joseph. 

Amesema, katika utekelezaji wa majukumu yao wameendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya rushwa wakiwemo waandishi wa habari, viongozi wa Serikali na wananchi kwa ujumla. 

Aidha, majukumu haya yametekelezwa katika wilaya zote zilizoko chini ya Mkoa wa Kagera. Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera, John K.E Joseph amesema, katika kipindi hiki cha miezi mitatu yaani kuanzia tarehe 1/10/2020 hadi 31/12/2020 TAKUKURU Mkoa wa Kagera wameweza kufanya kazi mbalimbali kama ifuatavyo;- 

UZUIAJI RUSHWA 

“Mojawapo ya majukumu ya TAKUKURU ni kushauri namna bora ya kuzuia na kupambana na rushwa na namna ya kutambua mianya ya rushwa katika mfumo na kuiondoa. 

Aidha, katika kutekeleza jukumu hili tumekuwa tukifanya ufuatiliaji na uchambuzi wa mifumo na kisha kushauri na wakati mwingine kuwezesha kurejeshwa kwa mali na au fedha ambazo zilikuwa zimufujwa au kuchukuliwa au kutaka kuchukuliwa visivyo halali.

“Katika kipindi tajwa tumeweza kuokoa jumla ya shilingi milioni mia tatu arobaini na moja laki tisa na moja mia tano sabini na senti sitini na mbili (sh. 341,901,570.62) fedha ambazo baadhi yake zilikuwa tayari zimechukuliwa visivyo halali na zingine zilikuwa katika mpango wa kuchukuliwa au kuibwa," 
amesema Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera, John K.E Joseph.

Aidha, sanjari na kufanya uokoaji na udhibiti wa fedha hizo pia amesema, wameweza kurejesha shamba lenye ukubwa wa ekari saba kwa mwananchi ambaye ni mkazi wa wilaya ya Biharamulo. 

Katika kiasi cha fedha kilichookolewa kiasi cha jumla ya shilingi milioni mia tatu na nne laki sita na moja mia tatu sabini na sita (sh.milioni 304, 601, 376) ni mali ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). 

Ufuatiliaji wa fedha hizi amesema, ulianzishwa mara baada ya kupokelewa kwa taarifa kutoka katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambapo katika ufuatiliji waliweza kubaini kuwa fedha hizo zilitokana na madeni hewa ambayo yalikuwa yamewasilishwa katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na maduka mawili ya madawa yakionyesha kuwa kati ya mwezi Mei na Novemba mwaka 2016 yalitoa madawa kwa wagonjwa yenye thamani ya kiasi cha fedha tajwa. 

"Hata hivyo ufuatiliaji wetu uliweza kubaini kuwa madai hayo yalikuwa ya uongo kwa kuwa Fomu za Bima ya Afya zilizowasilishwa zilikuwa zimeandikwa na mtu aliyedaiwa kuitwa Frida Samwel ambaye si Daktari na wala hakuwahi kuajiriwa katika Taaluma ya Udaktari katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera na hatambuliki, kwa maana hiyo nyaraka hizo zilikuwa zimegushiwa na ziliandaliwa kwa nia ovu ya kutaka kufanya udanganyifu. 

“Ufuatiliaji wetu uliweza kubaini pia kuwa maduka ya Madawa yaliyokuwa yamewasilisha madai hewa katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni MK PHARMACY linalomilikiwa na Murtaza Pathan lililokuwa limewasilisha hati za Madai zenye thamani ya Shilingi milioni mia mbili thelathini na moja laki tisa tisini na nne mia tano arobaini na nane (sh.231,994,548) na kulipwa shilingi milioni kumi laki moja tisini na nane mia sita themanini na tano (sh.10, 198, 685). 

“Hivyo kuendelea kudai jumla ya shilingi milioni mia mbili ishirini na moja laki saba tisini na tano mia nane sitini na tatu (sh. 221,795,863) na EJU ENTERPRISES linalomilikiwa na Erick Mugisha Kiiza lililokuwa limewasilisha hati za madai zenye thamani ya Shilingi milioni sabini na mbili laki sita na sita elfu mia nane ishirini na nane (Shs 72,606,828) na kulipwa kiasi cha shilingi laki moja sitini na tisa elfu mia nane (sh.169,800) na hivyo kuendelea kudai shilingi milioni sabini na mbili laki nne thelathini na saba elfu na ishirini na nane (Shs 72,437,028). 

“Katika ufuatiliaji wetu tumeweza kufanikisha kurejeshwa katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya fedha zote zilizokuwa zimelipwa yaani shilingi milioni kumi laki tatu sitini na nane mia nne themanini na tano (Tshs 10,368,485/=) kwa maduka haya mawili na vilevile tumewezesha kufutwa kwa madai yenye Jumla ya shilingi milioi mia mbili tisini na nne laki mbili thelathini na mbili mia nane tisini na moja (Shs 294,232,891/=) hayo kwani yalikuwa madai batili yaliyokuwa yameandaliwa ili kufanya ubadhilifu katika fedha za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,”amefafanua Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa,"amesema 

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera, John K.E Joseph amesema, pamoja na fedha hizo kurejeshwa pia kiasi cha shilingi thelathini na saba laki tatu mia moja tisi na nne na seti sitini na mbili (Shs 37,300,194/62) ni fedha zilizorejeshwa kwa makundi mbalimbali kama ifuatavyo;- 

-Benki ya Wakulima- KAGERA FARMERS COOPERATIVE BANK (KFCB) imerejeshewa kiasi cha shilingi milioni tisa laki tisa sitini na nne elfu mia nne tisini na nne na senti sitini na mbili (Shs 9,964,494.62) ambazo ni fedha zilizorejeshwa kutoka kwa wadiwa sugu na kuingizwa katika akaunti maalumu ya ukusanyaji wa madeni. 

-Chama kikuu cha ushirika cha wilaya ya Karagwe (KDCU) kimerejeshewa jumla ya shilingi milioni kumi na laki tano (Shs 10,500,000/=) feha hizi zimerejeshwa na watu waliokuwa wanaiba magunia ya chama hicho na kuyauza. 

-Halmashauri ya wilaya ya Karagwe imerejeshewa Jumla ya shilingi milioni saba na laki mbili (Shs 7,200,000/=) kutoka kwa Mkandarasi Sunday Robert Dionis aliyekuwa amelipwa fedha zaidi ya kazi aliyofanya katika mradi wa Maji. 

-Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa imerejeshewa Jumla ya shilingi milioni tatu laki saba elfu themanini na tano mia saba (Shs 3,785,700/=) kutoka kwa wadaiwa waliokuwa wamekopa fedha kutoka katika Akaunti ya Wanawake, Vijana na Walemavu 

-Kiasi cha Shilingi milioni tano laki nane elfu hamsini ((Shs 5,850,000/=) zimerejeshwa kwa Saccos za Jitihada, Biharamulo Saccos N.k. 

"Pia tumeweza kurejesha shamba moja lenye ukubwa wa ekari saba kwa Bw Liberius Yamkana shamba ambalo lilichukuliwa na Bw. Reuben Lutonja Sahani kama dhamana mara baada kukopesha shilingi laki moja (Shs 100,000/=) na kisha kuchukua shamba hilo na kuanza kulikodisha na kujipatia zaidi ya milioni nne laki mbili na elfu ishirini (Shs 4,220,000). 

Katika kipindi hiki cha miezi mitatu tumeweza kufanya tafiti nane (8) katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera na kufanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ishirini na mbili (22) yenye thamani ya jumla ya shilingi Bilioni sita milioni mia tatu ishirini na nane mia moja themanini na sita mia nane tisini na nne (shs 6, 328,186,894/=) miradi mingine tuliyofuatilia ni miradi ya ukarabati wa miradi ya maji, zahanati na ujenzi wa matundu ya vyoo, madarasa nk. 

Aidha tafiti hizo na ufuatiliaji ulilenga katika kutambua mianya ya rushwa ili kuwa katika nafasi nzuri ya kushauri,"amesema Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera, John K.E Joseph.

UCHUNGUZI 

Katika kipindi hiki cha miezi mitatu, tumeweza kufungua mashauri saba (9) mahakamani na wakati huo huo mashauri matano (5) yametolewa maamuzi mahakamani ambapo mashauri manne (4) watuhumiwa wake wametiwa hatiani na watuhumiwa wa mashauri moja wamekutwa hawana hatia. 

Ameema, kwa mashauri ambayo watuhumiwa wake hawakutiwa hatiani taratibu za kukata rufaa zinaendelea kwani hatukuridhika na maamuzi yaliyotolewa. Aidha, hadi sasa tuna jumla ya mashauri arobaini na sita yanayoendelea kusikilizwa mahakamani na yako katika hatua mbalimbali. 

Pia katika kipindi hiki tumeweza kukamilisha chunguzi mbalimbali ishirini na tatu (23). Pamoja na kukamilisha chunguzi hizo pia tunaendelea kufanya chunguzi mbalimbali na mojawapo ya chunguzi inayoendelea ni ya wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Kabale na VETA Bukoba zinazohusu uvujishaji wa mitihani kwa kutumia simu za mkononi na makundi ya WhatsApp. 

UELIMISHAJI UMMA 

Amesema, TAKUKURU Mkoa wa Kagera tunaamini kuwa Elimu ni tendo au uzoefu wenye athari katika akili, maarifa au maumbile ya mwanandamu na nyenzo muhimu katika kupitisha maarifa na maadili kutoka katika kundi moja kwenda kundi jingine, au kutoka katika kizazi kimoja kwenda kingine au kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine. 

Hivyo, ili kuongeza uelewa wa wana Kagera katika vita dhidi ya rushwa msisitizo wetu umekuwa katika kutoa Elimu katika makundi mbalimbali yenye kuhamasisha wananchi kutambua madhara ya rushwa, namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika maeneo ya kazi na biashara lengo likiwa ni kuifanya jamii ifahamu maana ya rushwa vyanzo vyake na madhara yake katika jamii. 

"Katika kuhakikisha elimu ya mapambano dhidi ya rushwa inawafikia watu wengi hapa mkoani Kagera, TAKUKURU imekuwa ikitoa Elimu kwa wananchi kwa kutumia njia mbalimbali hususani kupitia, vyombo vya habari, semina, mikutano ya hadhara, kushiriki maonyesho, michezo, nyimbo, mashairi, uandishi wa makala mbalimbali. Kwa sasa tunatarajia kufanya uelimishaji kupitia sanaa za maonyesho na ngoma za asili,"amesema Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera, John K.E Joseph. 

VIPAUMBELE KWA KIPINDI CHA JANUARI MPAKA MACHI 2021 

Pamoja na utekezaji wa majukumu yao ya kawaida pia, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera, John K.E Joseph amesema wamejiwekea malengo ya kutekeleza vipaumbele vifuatavyo:- 

I. Kuongeza kasi ya uchunguzi katika tuhuma kwenye vyama vya ushirika kwani katika vyama vya ushirika taarifa mbalimbali zinaonyesha kuna kuongezeka kwa vitendo vya rushwa na ufujaji wa mali za ushirika. Pamoja na kuongeza kasi katika maeneo ya miradi ya maendeleo, ubadhilifu katika makusanyo ya fedha za ndani za Halmashari kupitia utaratibu wa POS, na kufanya chunguzi katika miradi ya Afya. 

II. Kuongeza kasi katika kusimamia urejeshwaji wa fedha kutoka kwa wadiwa sugu wa iliyokuwa Benki ya Wakulima- KAGERA FARMERS COOPERATIVE BANK (KFCB) na kuhakikisha kuwa kila mdaiwa anarejesha fedha hizo haraka iwezekanavyo 

III. Kuongeza kasi ya uelimishaji umma kwa kutumia njia mbalimbali mfano kushiriki katika maonyesho na matamasha ya uelimishaji, semina, mikutano ya hadhara na mijadala ya wazi pamoja na kuendelea kufungua na kuimarisha klabu za wapinga rushwa mashuleni. Vilevile kutoa elimu kwa viongozi wa dini ili katika mahubiri yao waendelee kukemia vitendo dhidi ya rushwa. 

IV. Kuongeza kasi katika kufanya chambuzi za mifumo hasa katika maeneo yanayolalamikiwa zaidi hasa maeneo ya utoaji wa huduma kwa wananchi na katika miradi ya maendeleo hasa katika miradi ya maji ,ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na TARURA na katika utoaji wa vibali vya uwekezaji na uendeshaji wa vyama vya ushirika. 

V. Kutenga siku ya kusikiliza kero za wananchi kwa kila mwezi. Katika Mkoa wa Kagera tumejiwekea utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi walau mara moja kwa mwezi hii inamaanisha kuwa kila wilaya itakuwa na siku moja ya kusikiliza kero. 

"Zoezi hili litafanyika kwa kufika katika maeneo mbalimbali ya mitaa au vijijini kwa lengo la kusikiliza kero hizo. 

Tutakuwa tukitoa taarifa kwa wananchi kuwajulisha ni lini tukakuwa eneo Fulani. Kwa mfano mwezi huu wa Januari hapa Bukoba tutakuwa na zoezi la usikilizaji wa kero za wananchi siku ya tarehe 21.1.2021 katika Viwanja vya mashujaa. 

Lengo la kwenda katika maeneo mbalimbali na kufanya usikilizaji wa kero za wananchi ni kutaka kuzitambua kero zinazowakabili wananchi katika maeneo yao na kusaidia kuzitatua au kuwashauri jambo la kufanya ili kutatua kero hizo,"amesema Mkuu huyo. 

WITO

"Rushwa ni adui wa haki na inaweza kuathiri mgawanyo wa rasilimali katika jamii na kusababisha wananchi kukata tamaa. 

Hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuchukua hatua kila anapoona kuna dalili ya vitendo vya rushwa kufanyika na ni vyema kila mmoja wetu kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi zilizowekwa kwa maslahi mapana ya Taifa. 

Hivyo nitoe wito kwa Wananchi wote wa mkoa wa Kagera kuchukua hatua mahususi pale wanapoona kuna dalili au ukiukwaji wa sheria zetu za nchi au kuna viashiria vya uwepo wa vitendo vya rushwa,"Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera, John K.E Joseph

Post a Comment

0 Comments