TRA yawakamata 34 kwa kukaidi matumizi ya EFDs

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 2,108,203,163.70 sawa na asilimia 117 kati ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 1,798,607,033.71 katika kipindi cha miezi sita kutoka mwezi Julai hadi Desemba 2020 huku ikiwakamata watu 34 wakiwemo wafanyabiashara,wanunuzi wa bidhaa na watoa huduma mbalimbali kwa kosa la kutozingatia sheria, anaripoti Mwandishi Diramakini.Kaimu Meneja wa TRA Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Lewis Charles akitoa taarifa ya hali ya ukusanyaji mapato kwa kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2020 katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga ambapo mamlaka hiyo ilifanikiwa kukusanya zaidi ya bilioni 2 kati ya lengo la kukusanya bilioni 1.9. 

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka hiyo wilayani humo, Lewis Charles, wakati akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2020/2021 katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Mbinga (DCC) kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga. 

Aidha, amesema, katika mwaka wa fedha 2020/2021 TRA Wilaya ya Mbinga imepewa lengo la kukusanya shilingi bilioni 3.604 na malengo hayo yatafikiwa iwapo wananchi,wafanya biashara na wadau wengine watatoa ushirikiano kwa mamlaka hiyo. 

Kwa mujibu wa Lewis, katika kipindi hicho TRA imewakamata watu 34 wakiwemo wafanyabiashara,wanunuzi wa bidhaa na watoa huduma mbalimbali kwa kosa la kutozingatia matumizi sahihi ya mashine za Kielektroniki (EFDs) ambao wametozwa shilingi milioni 58,500,000 kama adhabu, kati ya hizo shilingi milioni 22,580,000 zimelipwa na milioni 35,920,000 zinategemewa kulipwa. 

Amesema, Mamlaka ya Mapato inaendelea kuwakumbusha wafanyabiashara na wananchi wote kwa jumla kuwa msingi wa makadirio ya kodi kwa haki ni utunzaji sahihi wa kumbukumbu na ni wajibu na kila mwenye sifa kulipa kodi stahiki za serikali. 

Lewis ameonya kuwa, mfanyabiashara yeyote atakayebainika kutotumia vyema mashine za kielektroniki katika biashara yake au kukaidi kutimiza wajibu huo wa kisheria atakuwa ametenda kosa na atachukuliwa hatua kali za kisheria. 

Amesema, mfanyabiashara atakayekamatwa kwa kosa la kutotumia mashine za EFDs adhabu yake ni faini kuanzia milioni tatu na isiyozidi milioni 4.5 au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja kwa mujibu wa sheria za usimamizi wa kodi ya mwaka 2015. 

Pia, amewataka wanunuzi wote wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha wanadai risiti pindi wafanyapo manunuzi kwani ni haki ya msingi na kisheria kwa kila mnunuzi, na kutofanya hivyo ni kosa linaloweza kupelekea kupata adhabu kali ikiwemo kutozwa faini kati ya shilingi 30,000 hadi milioni 1.5. 

Amesema, TRA inategemea sana ushirikiano kutoka kwa wadau wote katika suala zima la kukusanya mapato ya Serikali na kusisitiza,ni wajibu wa kila mwananchi kuonyesha uzalendo kwa kulipa kodi ili kuisaidia Serikali kutoa huduma bora na haraka zaidi. 

Lewis amesisitiza kuwa, ni haki na lazima kwa mwananchi kudai risiti sahihi kila anunuapo bidhaa au huduma pamoja na kutoa taarifa ya upotevu wa mapato ili kuiwezesha mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kuwahudumia Watanzania. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Kosmas Nshenye amewataka wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali katika wilaya hiyo kuhakikisha wanalipa kodi stahiki za serikali kwani suala la kodi ni lazima na kutoa ushirikiano kwa mamlaka ya mapato. 

Amesema, nchi zote zilizoendelea zimepiga hatua ya kiuchumi kutokana na mwamko mkubwa wa watu wake kulipa kodi na kuwaagiza watendaji wa mamlaka hiyo kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kufikiwa malengo waliyopewa na Serikali ya kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3 katika mwaka wa fedha 2020/2021.

No comments

Powered by Blogger.