UNESCO:Hongera Rais Dkt. Mwinyi, tutashirikiana na Serikali yako

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi ameipongeza azma ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulkia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi wa jengo la Beit al Ajaib baada ya kuporomoka sehemu kubwa ya jengo hilo hivi karibuni, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Mwakilishi Mkaazi wa UNESCO nchini Tanzania, Bw.Tirso Dos Santos alipowasili katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika leo Januari 13, 2021 na kulia ni Ofisa Utamaduni UNESCO Tanzania, Bi. Nancy Lazaro Mwaisaka.(Picha na Ikulu/ Diramakini).

Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Januari 13, 2021 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Tirso Dos Santos.

Rais Dkt. Mwinyi amemueleza Mwakilishi huyo wa UNESCO kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na shirika hilo, hivyo hatua yake hiyo ya kuinga mkono Zanzibar katika kulifanyia matengenezo jengo la Beit al Ajaib ni uthibitisho mkubwa.

Ameeleza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianza kuchukua hatua za makusudi mara tu baada ya kutokea tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuunda Kamati ya Uchunguzi ya sababu zilizopelekea kuanguka kwa jengo hilo la Beit al Ajaib huku yeye mwenyewe akikutana na wadau wa Mji Mkongwe kujadili tukio hilo kwa azma ya kutafuta ufumbuzi.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa ushauri kwa Shirika la UNESCO wa kuyafanyia tathmini majengo yote ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ili yasiendelee kuleta athari zaidi.

Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa, azma na utayari wa Shirika la UNESCO wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kulijenga jengo hilo la kihistoria ina umuhimu mkubwa katika kuurejeshea hadhi yake Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao upo katika urithi wa Dunia. 

Pia, Rais Dkt. Mwinyi amefurahishwa na azma ya shirika hilo la kuwaleta wataalamu kwa awamu tatu hapa Zanzibar ambapo kila awamu itakuwa na wataalamu wake ambapo inaonesha azma sahihi ya UNESCO ya kushirikiana na Zanzibar katika kulijenga tena jengo hilo kwa mtazamo wake wa asili na kwa kiwango kilicho bora zaidi.

Aidha, Dkt. Mwinyi amemueleza Mwakilishi huyo wa UNESCO kwamba Serikali anayoiongoza itahakikisha inatoa ushirikiano mkubwa kwa timu hizo za wataalamu watakaokuja kufanya shughuli hiyo hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira mazuri ya shughuli zao. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa UNESCO Nchini Tanzania, Bw.Tirso Dos Santos kulia kwa Rais wakiwa katika ukumbi wa Ikulu wakati wa mazungumzo yao yaliofanyika leo Januari 13, 2021 na kulia ni Ofisa wa Utamaduni UNESCO Tanzania, Bi. Nancy Lazaro Mwaisaka.(Picha na Ikulu/Diramakini). 

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi kwa upande mwingine amelipongeza shirika hilo kwa azma yake ya kulifanyia ukarabati jengo la sinema ya Majestic ambapo tayari nusu ya fedha za ujenzi huo kwa mujibu wa Mwakilishi huyo zimeshapatikana.

Ameeleza kuwa, shirika hilo limeweza kushirikiana na Zanzibar kwa muda mrefu hatua ambayo imepelekea kuimarika kwa miradi mbalimbali ambayo UNESCO inaiunga mkono ikiwemo miradi ya elimu, utamaduni, afya na mengineyo ambayo imepata mafanikio makubwa hapa Zanzibar.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kulipongeza shirika hilo kwa kuendelea kushirikiana na Zanzibar na kuahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na shirika hilo ili kutekeleza malengo yaliokusudiwa.

Mapema Mwakilishi huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Tirso Dos Santos amemueleza Rais Dkt. Mwinyi kuwa shirika hilo lina azma ya kulifanyia maboresho ya ujenzi jengo la Beit-al -Ajaib ili lirudi katika uhalisia wake kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mwakilishi huyo alimueleza Rais Dkt. Mwinyi kuwa,shirika hilo litaanza kuleta wataalamu wake kwa ajili ya mradi huo ambao wataanza kuja Januari 18, mwaka huu ambao watakuja kwa awamu tatu ili kuhakikisha lengo lililokusudiwa linafanikiwa tena kwa muda uliopangwa na ufanisi mkubwa.

Alimueleza Rais Dkt. Mwinyi kwamba UNESCO itahakikisha inafuata taratibu zote katika kuhakikisha ujenzi huo ufanywa kwa taratibu zote za Kimataifa bila ya kuathiri mambo mengine.

Pia, Mwakilishi huyo wa UNESCO amemueleza Rais Dkt. Mwinyi kwamba baada ya timu hizo za wataalamu kukamilisha kazi zao ujenzi wa jengo hilo utaanza mara moja huku akimueleza kuwa amepokea ushauri na wazo la kuyafanyia tathimini majengo ya Mji Mgongwe wa Zanzibar.

Pamoja na hayo, Mwakilishi huyo wa UNESCO, alimueleza Rais Dkt. Mwinyi kwamba shirika hilo liko tayari kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la sinema ya Majestic ambalo limo katika Mji Mkongwe wa Zanzibar na tayari nusu ya fedha za ukarabati wa jengo hilo ziko tayari.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiagana na mgeni wake Mwakilishi Mkaazi wa UNESCO Nchini Tanzania, Bw. Tirso Dos Santos. Kulia kwa Rais baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mhe.Lela Mohammed Mussa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said na kulia ni Ofisa Utamaduni wa UNESCO Tanzania, Bi. Nancy Lazaro Mwaisaka.(Picha na Ikulu/Diramakini).

Mwakilishi huyo alimpa salamu za rambirambi zilizotumwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Audrey Azoulay pamoja na Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Urithi wa Dunia, Mechtild Rossier kufuatia kuporomoka kwa jengo la Beit al Ajaib na kupelekea vifo pamoja na mejeruhi kadhaa. 

Sambamba na hayo, kiongozi huyo alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kwa kuadhimisha miaka 57 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 huku akisisitiza UNESCO itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi yake mbalimbali ili iweze kuleta tija na ufanisi.

Sehemu kubwa ya jengo la Beit el Jaaib lililopo Forodhani jijini Zanzibar ambalo ni miongoni mwa majengo ya urithi wa Dunia ambapo pia, ni miongoni mwa majengo yanayotambuliwa na UNESCO liliporomoka Ijumaa ya Disemba 25, mwaka jana 2020 likiwa linaendelea kufanyiwa ukarabati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news