BITEKO AWATAKA BUKREEF KUKAMILISHA MASHARTI YA SERIKALI ILI WAPEWE LESENI YA UCHIMBAJI

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameitaka kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Bukreef ambayo inafanya kazi kwa ubia na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na kampuni ya Tanzam kukamilisha masharti waliyopewa na Serikali ili wapatiwe leseni ya uchimbaji,anaripoti Tito Mselem (WM).
Waziri wa Madini, Doto Biteko (katika), kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya na kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila wakiwa kwenye Kikao na Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Bukreef kilichofanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)

Waziri Biteko ameyasema hayo alipofanya kikao na wawakilishi wa kampuni hizo kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Amesema, Bukreef wanapaswa kulipa fidia kwa watu wote wanaotakiwa kulipwa pamoja na kuwasilisha taarifa ya fedha ya kibenki (bank statement) ili wizara pamoja na Tume ya Madini ijiridhishe kama kweli kiasi hicho cha fedha wanacho.

Imeelezwa kuwa, mkataba baina ya Bukreef na STAMICO haukuwa wenye usawa, kwa sasa mikataba hiyo imerekebishwa ambapo STAMICO wameridhika na mkataba huo.

Aidha, mkataba huo, unawapa kipaumbele STAMICO katika kazi ya uchorongaji ambapo mkataba huo utakuwa na maslahi mapana kwa Taifa.
Pia, Waziri Biteko amesema, Mabadiliko ya Sheria ya Madini yameleta chachu ya maendeleo katika Sekta ya Madini ambapo amewataka Bukreef kulipa fidia na kuwasilisha haraka mpango wa uzalishaji ili kazi zianze kufanyika.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Tanzam, Khalaf Rashid amesema, kampuni ya Bukreef ilikuwa inayumba, lakini baada ya kuanza kushirikiana kwa pamoja, tumeanza kuonesha mafanikio ambapo kampuni inaamini itazalisha kwa faida.

“Nichukue fursa hii kuwaomba viongozi wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini, kwamba mtupunguzie masharti mliyotupa kama kuanza uzalishaji ndani ya miezi sita pia kumaliza zoezi la kuwalipa fidia wenye maeneo yao ndani ya kipindi cha miezi sita,”amesema Rashid.

Rashid aliongeza kuwa, Mgodi wa Bukreef ulitenga zaidi ya dola za Marekani bilioni 25 kwa ajili ya kazi ya uchimbaji mara baada ya kuruhusiwa.

Pia Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema, katika utoaji wa leseni, Sheria ya Madini inaonesha wazi kuwa kila kwenye mita moja ndani ya eneo la leseni unatakiwa uwe na kiasi cha fedha kisicho pungua dola za Marekani 500.

Katika hatua nyingine, kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya MMC ya mkoani Morogoro imeeleza kuwa, mpaka sasa imewekeza zaidi ya bilioni 30 katika eneo ambalo walitengewa wachimbaji wadogo ambapo wanauhakika wa kuzalisha kilo 30 za dhahabu kwa mwezi endapo watapatiwa leseni ya uchimbaji katika eneo hilo.
Baadhi ya washiriki walioshiriki Kikao cha Waziri wa Madini Doto Biteko na Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Bukreef kilichofanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Aidha, uongozi wa kampuni hiyo umemueleza Waziri wa Madini kuwa, mpaka sasa kampuni hiyo imetoa zaidi ya ajira 300, imechangia ujenzi wa barabara na imetoa ahadi ya kujenga kituo cha afya pamoja na shule katika eneo linalozunguka mgodi huo.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya amewataka wawekezaji kufuata kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa na Serikali wakati wanapohitaji leseni ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima.

Pia Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amesema, maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo lazima wachimbe wachimbaji wadogo vinginevyo inatakiwa kampuni husika ielewane na wachimbaji waliokuwepo ili wachimbe kwa kushirikiana na Wizara ijiridhishe ndiyo Tume itaweza kutoa leseni kwenye maeneo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news