Maalim Seif Sharif Hamad afariki dunia

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi  ametangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kilichotokea leo Februari 17, 2021 mnamo majira ya saa 5:26 asubuhi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Akitangaza kutokea kwa msiba huo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amefariki dunia wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa tokea tarehe 9 Februari, 2021.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ni Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar.

"Kwa niaba ya wananchi, nachukua fursa hii kutoa pole na salamu zangu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, Chama cha ACT-Wazalendo na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania na kuwataka wawe na subira na ustahamilivu katika kipindi hiki cha majonzi,"amesema Rais Dkt. Mwinyi katika taarifa hiyo.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa hakika Taifa limepoteza kiongozi Mzalendo na shupavu.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi katika taarifa hiyo maalum ya tanzia ameeleza kuwa taarifa zaidi za msiba huo na maziko yake zitaendelea kutolewa na Serikali kwa ushirikiano wa karibu na familia pamoja na chama cha ACT-Wazalendo.
Rais Dkt. Mwinyi alimuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahala pema peponi. Amin.
Aidha, kupitia ukurasa wa Twitter, Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli atoa salamu za rambirambi

"Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Natoa pole kwa Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Mwinyi, Familia, Wazanzibari, wanachama wa ACT-Wazalendo na Watanzania wote. Mungu amweke mahali pema peponi,Amina"

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news