Mshikamano wahitajika kuokoa mamilioni ya wanawake waliopo hatarini kukeketwa

Umoja wa Mataifa umetaka ushirikiano katika ngazi zote na katika sekta zote za kijamii ili kulinda mamilioni ya wasichana na wanawake walio hatarini kukumbwa na ukeketeaji kila mwaka.

Wakati huo huo, umuhimu wa ushirikiano huo umetajwa kuwa na nafasi kubwa zaidi kutokana na hofu kuwa ukeketaji wa watoto wa kike na wanawake milioni mbili unaweza kufanyika katika muongo ujao.

Ni wakati huu ambapo janga la ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) limesababisha shule kufungwa na kuvuruga mipango mingine ya ulinzi wa kundi hilo dhidi ya ukeketaji.

Katika ujumbe wake wa siku ya Kimataifa ya kupinga ukeketaji, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres aliangazia kuwa kwa kushirikiana kuwa, “kwa pamoja tunaweza kutokomeza FGM ifikapo mwaka 2030.

“Wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unaingia katika muongo wa hatua za utekelezaji wa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, hebu na tuufanye muongo huu kuwa muongo wa kutokuwepo kwa vitendo vya ukeketaji,”amesema Guterres.

Katibu Mkuu amesema, kwa kufanya hivyo Dunia itavuna mafanikio chanya kwenye afya, elimu na maendeleo ya kiuchumi kwa wanawake na watoto wa kike.

Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la Kuhudumia Watoto la UNICEF na lile la idadi ya watu, UNFP nao pia walisema kuwa, kutokomeza ukeketaji watoto wa kike na wanawake na kufanikisha usawa wa jinsia ni mambo mawili yanayoimarisha malengo ya SDGs.

“Hebu weka tu kwamba usawa wa jinsia ungalikuwa ni kitu kipo, kusingalikuwepo na FGM. Hii ni dunia tuitakayo,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore na Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Natalia Kanem katika taarifa yao ya pamoja.

Wametaka ushirikiano thabiti na umoja katika ngazi zote na sekta zote sambamba na upatikanaji wa fedha za kutosha ili kulinda na kunusuru wanawake na wasichana walio hatarini kukeketwa.

“Tunafahmau kile kinachowezekana. Tumevumilia visingizio. Tumechoshwa na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. Ni wakati wa kuungana kupitia mikakati iliyoidhinishwa, tuipatia ufadhili wa kutosha na tuchukue hatua,” wamesisitiza.

Aidha, FGM ni kitendo hatari, dhalili na kinachukia ambacho ni sawa na ukiukwaji wa haki za binadamu. Kitendo hiki kinahusisha kuondoa sehemu au kuondoa kabisa eneo la siri la mwanamke bila sababu zozote za kitabibu.

Katika tamaduni ambako kitendo hicho kinaungwa mkono, mara nyingi hufanywa na mtabibu wa kiasili akitumia vifaa katili na bila dawa ya kuzuia maumivu.

Matokeo yake ni madhara ya kiafya kimwili na kiakili kwa wanawake na wasichana. Madhara makubwa ni pamoja na kuvuja damu kupitiliza, kuhabika kwa njia ya mkojo, maumivu wakati wa tendo la ndoa na hata kuchanika kwa sehemu za njia ya mkojo na haja kubwa wakati wa kujifungua.

Dkt.Kanem alisema, hata katika nchi ambako ukeketaji unapungua, bado harakati zinapaswa kuongezwa mara 10 ili kufikia lengo litakiwalo mwaka 2030.

“Kufikia lengo hilo kunahitaij dola bilioni 2.4 katika kipindi cha miaka 10 ijayo, sawa na chini ya dola 100 kwa kila mtoto wa kike. Hii ni gharama ndogo sana ambayo inahitajika ili kutunza utu, afya na haki ya mtoto wa kike,”amesema.

Fore na Dkt. Kanem walisisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano kwa mapana zaidi wakiwemo wadau mbalimbali kama vile wanaume na wavulana pamoja na mashirika ya kidini, taasisi za kusimamia sheria na haki na mahakama.

Aidha, ikiadhimishwa kila mwaka tarehe 6 mwezi Februari, siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji watoto wa kike na wanawake, inalenga kupazia sauti juhudi za kuondokana na FGM na ilitangazwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2012.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news