Rais Magufuli afichua siri ya Balozi Kijazi, Maalim Seif ataka watu waache kutishana

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William Kijazi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.
 
Wakati wa tukio hilo la kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John William Kijazi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli amesema Taifa limempoteza mtu muhimu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
 
Huku akianisha kuwa, marehemu Balozi Kijazi alikuwa mchapa kazi, kwani hata awali alikosa mtu wa kumteua kuwa Katibu Mkuu kiongozi baada ya aliyekuwa akishika nafasi hiyo, Balozi John Kijazi kustaafu mwaka 2017 na hivyo kuamua kumuongezea muda tena.

Rais Magufuli amesema hayo Februari 19, 2021 katika ibada ya mazishi ya Balozi Kijazi aliyefariki dunia usiku wa Februari 17, 2021 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa alikokuwa akipatiwa matibabu jijini Dodoma.

Aidha, Rais Magufuli amesema Balozi Kijazi aliyezaliwa mwaka 1956 umri wake wa kustaafu ulifika mwaka 2017 na alilazimika kuendelea kufanya naye kazi kutokana na kukosa mbadala wake.

“Alizaliwa mwaka 1956, lakini mpaka leo alikuwa bado ni katibu mkuu kiongozi, maana yake ulipofika wakati wa kustaafu mwaka 2017 nikajaribu kuangalia nani wa kuchukua nafasi yake nikakosa.

“Nikamuongeza miaka miwili nikifikiri ndani ya muda huo nitapata mwingine, lakini hadi mwaka 2019 sikupata, nikamuongeza tena miaka mingine miwili, Mungu akasema umezoea kweli akamtumie yeye mwenye,”amesema  Rais Dkt.Magufuli.

Pia ametumia nafasi hiyo kutoa pole kwa familia, mke wa marehemu na  watoto huku akibainisha kuwa Kijazi alikuwa mtu mwenye upendo mkubwa na alimpenda Mungu na siku za Jumapili hakukosa kwenda kanisani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William KijaZi katika
viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.
 
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kumuomba Mungu ili kuliepusha Taifa dhidi ya virusi vya ugonjwa wa Corona (COVID-19) na kusisitiza kuwa hatatangaza kuwafungia watu ndani.

"Tusitishane na kuogopeshana Mungu yupo, Mungu ndiyo muweza wa yote, Tuendelee kusimama na Mungu, tulishiinda Corona mwaka jana. Naomba Tusimame na Mungu.

"Magonjwa yapo na yataendelea kuwepo, magonjwa ya vifua, magonjwa ya kupumua na kadhalika yatakuwepo na hayakuanzia hapa, Zipo Nchi ambazo zimepoteza watu wake wengi. Sisi Tanzania Mungu ametusaidia sana mwaka uliopita, tuendelee kuchukua tahadhari huku tukimuomba Mungu. Mungu hashindwi,"amesema Rais Dkt.Magufuli.

"Naomba tusitegemee nguvu za ubinadamu, bali tumtegemee Mungu. Narudia ndugu zangu tujue Mungu yupo. Mungu ndiyo muweza wa yote. Nashukuru viongozi wa dini mmeendelea kulihubiri hilo. Tuendelee ndugu zangu kusimama na Mungu. Tulishinda mwaka jana, inawezakana hili ni jaribu jingine, nalo tukisimama na Mungu tutashinda,"ameongeza.
Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu wakuu wakijiandaa kwenda kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William KijaZi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021."Tusitishane na kuogopeshana, tutashindwa kufika. 
 
"Inawezekana kuna mahali tumemkosea Mungu. Inawezeakana kuna mahali tunapata jaribu kama wana wa Israel walivyokuwa wanaenda Kaanani. Tusimame na Mungu ndugu zangu Watanzania. Kufa tutakufa tu,unaweza kufa kwa malaria,ukafa kwa Kansa,ukafa kwa magonjwa mengine kwa sababu kufa kupo lakini Kamwe tusimuache Mungu. Huo ndiyo wito wangu.

"Tusimame na Mungu ndugu zetu Waislamu walitangaza muda wao wa kuomba na niliambiwa na Mufti,niwaombe tena Watanzania kama kuna mahali tumetetereka tuendelee kumuomba Mungu. Tuanze leo kwa ndugu zetu Waislamu,kesho Jumamosi kwa ndugu zetu Wasabato wanaosali Jumamosi na Jumapili kwa ndugu zetu Wakristo kwa kumuomba kufunga kwa siku tatu. Mimi nina uhakika tutashinda. Nataka niwape nguvu hiyo ndugu zangu Watanzania,"ameongeza Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli akiongoza kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William Kijazi katika
viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.
 
"Naomba viongozi wa dini muendelee kusisitiza maombi. Tulishinda mwaka jana, tutashinda mwaka huu, tutashinda miaka yote kwa sababu kamwe Mungu hajaweza kuliacha taifa hili.Tumeshinda mwaka jana na tukaingia kwenye uchumi wa kati na Corona ipo,uchumi ukaendelea kupanda na Corona ipo,miradi ikaendelea kutekelezwa wala hatukuweka Lockdown hata sasa hatutaweka Lockdown kwa sababu tunajua Mungu yupo siku zote. Taifa hili lipo mikononi mwa Mungu,"amesema Rais Magufuli.

Mbali na hayo, Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ameeleza kusikitishwa na watu wanaozusha taarifa za uongo kwamba Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amefariki dunia huku akisoma ujumbe mfupi aliotumiwa na Waziri Dkt. Mpango kuhusu hali anayoendelea nayo.

"Imefikia mahali sasa tunatishana sana. Leo asubuhi nilitumiwa meseji na Waziri wa Fedha, Dkt. Mpango ambaye amelazwa Dodoma na ninaomba niiosome hapa kwa faida ya wale waliokuwa wana 'Twiti' kwamba amekufa,"amesema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William KijaZi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.

Rais Magufuli amesema katika ujumbe huo, Dkt. Mpango amemueleza kuwa kwa neema ya Mungu anaendelea vizuri, anakula vizuri na anaendelea kufanya mazoezi ya kifua na kutembea na kwamba wale waliomzushia mtandaoni kuwa amefariki dunia amewaombea kwa Yesu wakati wa sala ya jioni jana.

“Mheshimiwa Rais, asante sana nimepata ujumbe wako kupitia kwa mke wangu, kwa neema ya Mungu naendelea vizuri, ninakula, ninafanya mazoezi ya kifua na kutembea, hao wanaonizushia kifo kwenye mitandao niliwaombea msamaha kwa Yesu wakati wa sala ya jioni jana.”

“Mheshimiwa Rais Mungu akubariki na akupe neema na ujasiri zaidi katika kuliongoza Taifa letu, katika wimbi hili naungana na wanafamilia katika kuomboleza kifo cha Katibu mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Rest in Peace,” amesema Magufuli akimnukuu Dk Mpango.

Akifafanua kuhusu ujumbe huo Magufuli amesema, “ni huyo ambaye aliambiwa jana amekufa, yeye amesema katika sala yake jana jioni aliwaombea msamaha kwa Yesu.”

“Magonjwa yapo na yatendelea kuwepo, magonjwa ya kupumua na vifua pia yataendelea kuwepo na hayakuanzia hapa kwani zipo nchi zilizopoteza watu wengi lakini Tanzania Mungu ameisaidia katika mwaka uliopita,"amesema.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli akiongoza kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William KijaZi katika
viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.
 
Wakati huo huo akimzungumzia aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alifariki dunia Februari 17, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu na kuzikwa jana Mtamwe wilayani Wete kisiwani Pemba, Zanzibar, Rais  Dkt. Magufuli amesema baada ya kufanya mazungumzo naye wakati wa uhai wake alibaini kuwa Maalim Seif alikuwa ni kiongozi wa tofauti sana.

“Maalim Seif alikuwa ni kiongozi wa tofauti sana mwaka 2015 nilipokuwa rais baada ya uchaguzi wa Zanzibar kufanyika ule wa marudio, Maalim Seif aliniandikia barua akiniomba kuja kuniona nilisita kidogo kwamba kwa nini anataka kuja kuniona na wakati hata kwenye uchaguzi hakushiriki, Maalim Seif akaandika tena barua ya pili na baadaye akaandika barua ya tatu.

“Kila nilipokuwa najaribu kupata ushauri kutoka Zanzibar nilikuwa naambiwa nisubiri nimuache, lakini baadaye nikaamua ngoja nimuone Maalim Seif. Alipokuja Ikulu Dar es Salaam nilipoanza kuzungumza naye nilimuona mtu tofauti sana na jinsi picha ilivyokuwa imejengeka kwa sababu mazungumzo yetu yalikuwa mazuri sana,”ameeleza Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli akiongoza kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William KijaZi katika
viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.

Rais Magufuli amesema, Maalim Seif alimueleza kuwa hakushiriki kwenye uchaguzi wa marudio Zanzibar uliofanyika Machi, 2016 baada ya ule wa Oktoba 25, 2015 kufutwa akisisitiza kuwa licha ya jambo hilo kutokea, lakini Zanzibar itakuwa salama na kwamba hatohamasisha fujo.

Akiendelea kumnukuu Maalim Seif, Rais Magufuli amesema kuwa,“Pili lakini nataka kukuhakikishia Zanzibar itakuwa salama sitahamasisha fujo yoyote na miaka yote mitano aliyechaguliwa ataendelea vizuri kutawala kauli hiyo niliiona mpaka baada ya miaka mitano alieleza yeye anapenda amani na angependa Zanzibar na Watanzania wote wakae kwa amani, kauli hiyo niliithibitisha kwa vitendo ulipotokea uchaguzi mwingine Maalim Seif bado alishiriki katika Serikali ya Muungano, Serikali ya Umoja wa Kitaifa".
Katibu Mkuu Ikulu Dkt. Moses Kusiluka akiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Bi. Dorothy Mwaluko wakibeba shada la maua lenyen herusi KMK yaani Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi
Balozi John William KijaZi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.  (Picha zote na Ikulu).

“Alikuwa ni mtu mcheshi na siku zote katika ziara yake hata kule Chato alikuwa akihubiri umoja wa Wanzanzibar umoja wa Watanzania kitu ambacho amemaliza nacho, Maalim Seif amemaliza salama na dhamira yake ya kuijenga amani na Wazanzibari na Watanzania kwa pamoja,”amesema.

“Natoa pole kwa Watanzania wote kwa vifo vyote viwili, cha Maalim Seif pamoja na cha Balozi Kijazi, Jana nilimtuma Makamu wa Rais na Dkt. Bashiru waniwakilishe kwenye mazishi ya Maalim Seif". Kijazi ameondoka hapa duniani kama Shujaa, Maalim Seif kaondoka hapa duniani kama shujaa.
 
“Balozi Kijazi na Maalim Seif wametangulia zamu yetu sisi bado, Watanzania katika matatizo yoyote yanapotokea yatufanye tuwe wamoja, hofu ni mbaya, ukiona kitu hauwezi kukitatua wewe, mwambie Mungu ndiye muweza, tumekuwa tunatishana sana, tusitishane,"amesema Rais.
 
Zanzibar
 
Awali wakati wa maziko, akisoma wasifu wa marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera na Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema kuwa Marehemu Maalim Seif alizaliwa tarehe 22 Octoba mwaka 1943 , Mtambwe Nyali na alipata elimu ya Msingi katika Skuli ya Uondwe na Skuli ya Wete Boy’s huko Pemba kati ya mwaka 1950 – 1957.

Alieleza kuwa Maalim Seif alisoma Elimu yake ya Sekondari kuanzia mwaka 1958 hadi 1961 katika Skuli ya King Geoge VI Memorial mjini Zanzibar ambayo kwa sasa ni Skuli ya Sekondari ya Lumumba na aliendelea na masomo ya cheti cha cha sekondari katika skuli hiyo.

Mwaka 1972 -1975 , alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar-es –Salaam kwa masomo ya Shahada ya Kwanza katika fani ya Sayansi ya Siasa, Utawala wa Umma na Ushirikiano wa Kimataifa na kutumikia Digrii ya Heshima (BA honours)mwaka 1975.

Marehemu Maalim Seif Sharif alikuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri wa Elimu kuanzia mwaka 1977 hadi 1980 na kubahatika kuwa mmoja wa Wajumbe waanzilishi wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar mwaka 1980 na kuendelea hadi mwaka 1989 na mwezi Februari, 1984-1988 alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar.

Waziri Khalid alimuelezea Marehemu Maalim Seif jinsi alivyoanzisha chama cha CUF na baadae kujiunga na ACT Wazalendo mnamo Machi 2019 sambamba na kuteuliwa kuwa Makamo wa Kwnaza wa Rais aliyoishikilia kaunzia Novemba 9,2010 hadi Machi 2016.

Pia, Marehemu aliteuliwa tena kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais kufuatia kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, na kuteuliwa kushika nafasi hiyo tarehe 7 Disemba nafasi ambayo aliishikilia hadi alipofikwa na mauti jana (tarehe 17 Februari,2021). Marehemu ameacha kizuka na watoto wanne.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news