TCRA yasitisha utoaji leseni za maudhui mtandaoni

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kusitisha utoaji wa leseni za Maudhui Mtandaoni kwa muda kuanzia Januari 28,2021 hadi Juni 30,2021, anaripoti Kadama Malunde (Malunde 1 blog).
Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Mihayo akizungumza kwenye Usiku wa Waandishi wa Habari na Wadau wa Habari Kanda ya Ziwa katika ukumbi wa Gold Crest Hotel Jijini Mwanza.

Akizungumza usiku wa kuamkia leo Februari 2,2021 kwenye Usiku wa Waandishi wa Habari na Wadau wa Habari Kanda ya Ziwa katika ukumbi wa Gold Crest Hotel jijini Mwanza, Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Mihayo amesema hatua ya kusitisha utoaji leseni kwa Blogs na Online Tv inatokana na kuendelea kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa matumizi sahihi ya mtandao.

“Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuanzia tarehe 28 Januari, 2021 imesitisha utoaji leseni za maudhui mtandaoni kwa muda hadi tarehe 30 Juni 2021 ili kutoa fursa kwa TCRA kufanya tathmini na kuja na hatua muhimu za kurekebisha dosari nyingi zilizojitokeza,”amesema Mhandisi Mihayo.

Mhandisi Mihayo pia amewataka watoa huduma wa sekta ya utangazaji kutekeleza matakwa ya kanuni ya uendeshaji ikiwemo kuwalipa mishahara watumishi wao.

Aidha, amewasihi waandishi wa habari kupendana na kushirikiana na kuhakikisha wanajiendeleza kielimu kuanzia ngazi ya Diploma ili kukidhi vigezo vinavyotakiwa.

1 comment:

  1. Asanteni kwa taarifa. Nawapenda sana nduguzangu

    Karibuni katika blog yangu changa

    www.mrbunduki.com

    ReplyDelete

Powered by Blogger.