Yanga SC yatoshana nguvu na Mbeya City

Wanajangwani, Yanga SC wamelazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji, Mbeya City jioni ya leo Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Yanga SC inayofundishwa na kocha Mrundi, Cedric Kaze leo ilikuwa inaondoka na ushindi kwa bao la Deus Kaseke dakika ya 84, kama si Mbeya City kusawazisha kwa penalti dakika ya 90 kupitia kwa Pastory Athanas.

Refa Ludovick Charles aliwapa penalti Mbeya City dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 kufuatia kushauriana na msaidizi wake namba mmoja, Ferdinand Chacha, wote wa Mwanza wote wakijiridhisha beki wa Yanga, Yassin Mustapha aliunawa mpira kwenye boksi.

Aidha, mshambuliaji Pastory Athanas akaenda kuisawazishia Mbeya City kwa mkwaju wa penalti uliompita kipa, Metacha Boniphace Mnata.

Wachezaji wa Yanga SC waliwafuata marefa kuwazonga baada ya mchezo huo kabla ya kuzuiwa na viongozi wao akiwemo kocha Msaidizi, Nizar Khalfan.

Dakika 45 za kwanza za mchezo huo zilimalizika kwa timu hizo kutofungana na kipindi cha pili zikiwa zimesalia dakika sita kabla ya filimbi ya mwisho, mtokea benchi Deus Kaseke akaifungia Yanga SC bao la kuongoza.

Zilikuwa ni juhudi binafasi za Kaseke aliyepasua katikati ya mabeki wa Mbeya City kabla ya kufumua shuti ambalo mabeki wa wenyeji walijaribu kuokolea ndani, lakini refa Ludovick Charles akawa makini.
 
Februari 12, 2021 Ihefu FC ya Mbarali mkoani Mbeya limewaadhibu wenyeji, Ruvu Shooting kwa kuwachapa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Mabao ya Ihefu SC inayofundishwa na Zubery Katwila yamefungwa na Issa Ngoah yote dakika ya 21 na 90 na ushei na kwa ushindi huo inafikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi 19 na kusogea nafasi ya 16 katika ligi ya timu 20, ikiizidi pointi mbili tu Mbeya City inayoshika mkia kwa sasa.

Ruvu Shooting iliyo chini ya kocha mzoefu, Charles Boniface Mkwasa inabaki na pointi zake 28 za mechi 19 sasa katika nafasi ya tano.

Pia katika mechi iliyotangulia, Tanzania Prisons imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya KMC Uwanja wa Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa.

Mabao ya Prisons yalifungwa na Jeremiah Juma Mgunda dakika ya 29 na 59, wakati la KMC limefungwa na Israel Patrick Mwenda dakika ya 37.

Prisons inafikisha pointi 25 baada ya kucheza mechi 19 na kupanda nafasi ya saba, wakati KMC inabaki na pointi zake 25 za mechi 19 pia katika nafasi ya sita.

No comments

Powered by Blogger.