Zanzibar yaonyesha msimamo kukomesha vitendo vya udhalilishaji

Jamii nchini imeshauriwa kuwa na msimamo wa pamoja katika kupinga vitendo vya udhalilishaji vilivyoshamiri ndani ya visiwa vya Zanzibar ili kupunguza machungu kwa waathirikka wa vitendo hivyo wakiwemo wanawake na watoto, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Makamu wa Pili wa Pili wa Rais, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alitoa ushauri huo mara baada ya kukamilika kwa ibada ya sala ya Ijumaa katika Masjid ya Al-Twarika katika kijiji cha Karange Donge wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mhe. Hemed alieleza azma ya seriakli ya awamu ya nane imelenga kuvitokomeza vitendo hivyo ambapo hivi karibuni imechukua jitihada za maksudi kwa kuifanyia marekebisho sheria ya makosa ya udhalilishaji kwa lengo la kuondoa mianya ya kupatiwa dhamana watendaji wa makosa hayo.

Makamu wa Pili wa Rais amesema, Zanzibar imebarikiwa na neema kubwa ya kuwepo kwa wanawake hivyo jamii haina budi kuchukua maamuzi sahihi ya kufunga ndoa kwa lengo la kuondosha changamoto iliopo sasa katika jamii.

Aidha, amesema masuala ya udhalilishaji yanapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote kwani tayari yameshaleta athari kubwa kwa jamii na kueleza kuwa endapo hazitachukuliwa hatua za maksudi basi kuna uwezekano wa kupoteza nguvu ya Taifa katika siku za Usoni.

“Mhe. Rais hapendi kuongoza Nchi ikiwa na vitendo vya udhalilishaji kwani vinaabisha jamii yetu,” ameeleza Makamu wa Pili wa Rais.

Akizungumzia suala la Amani na Utulivu Mhe. Hemed aliwaeleza waumini hao kuwa hawana budi kuiendeleza na kuienzi tunu hii ya taifa kutokana na mchango wake wa kushajihisha kupatikana kwa maendeleo sambamba na kuiwezesha jamii kutekeleza mambo ya kijamii ikiwemo masuala ya ibada.

Amesema, madhehebu ya dini zote nchin yanahimiza juu ya umuhimu wa umoja, mshikamano na utunzaji wa Amani hali inayowapa uhuru na wasaa mzuri waumini katika kutekeleza ibada.

“Ndugu waumini wenzangu zipo nchi kadhaa duniani zimekosa hata kuitekeleza sala ya Ijumaa kama tulivyo sisi hapa kwa sababu ya kukosa Amani katika nchi zao,"amefafanua Mhe.Hemed.

Akimalizia nasaha zake, Makamu wa Pili wa Rais aliwaomba waumini hao kuendelea kumuunga mkono Mhe. Rais kwa kuacha makatazo yote yalioanishwa na serikali ikiwemo vitendo vya rushwa, wizi, ubadhilifu, Uzembe pamoja na Udhalilishaji.

Nae Ustadhi Haji Ali Makame aliwasihi waumini kutimiza wajibu wao kwa kuendelea kushikamana na kushirikiana katika kuzidisha mapenzi miongoni mwao ili kupata matunda mema hapa duniani na kesho Akhera.

Amesema, waumini lazima waepukane na vitendo vya farka ili kumpa ushirikiano Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi juu ya dhamira yake njema ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Waumini hao wa Masjid Al- Twarika walifanya dua maalum ya kumuombea Mhe. Rais wa Zanzibar ili Mwenyenzi Mungu ampe nguvu za kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.

Mapema, Mhe. Makamu wa Pili wa Raisi alifika nyumbani kwa Mzee Ali Ameir kumjulia hali na kubadilisha nae mawazo.

Katika mazungunzo yao Mzee Ali Ameir alimuomba Makamu wa Pili wa Rais kumfikishia salamu zake za dhati za kumpa pole Mhe. Rais kwa kuondokewa na Makamu wake wa kwanza marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.

Post a Comment

0 Comments