Ajali ya basi yaua sita, yajeruhi 19 wilayani Babati

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishina Msaidizi Mwandamizi Paul Kasabago amethibitisha kuwa, ajali ya basi la Kampuni ya Machame Investment imeua watu sita na kujeruhi 19, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Babati).

Ni baada ya basi hilo kupata ajali leo Machi 30, 2021 katika Kijiji cha Kiongozi kilichopo wilayani Babati Mkoa wa Manyara.
Aidha, Kamanda Kasabago amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo ila uchunguzi wa awali unaonyesha ni mwendo kasi na miili ya marehemu hao imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Mrara mjini Babati huku majeruhi nao wakiendelea na matibabu hospitalini hapo.

Basi hilo lilikuwa safarini kutoka Dodoma kwenda mjini Moshi kupita jijini Arusha, ambapo kwa mujibu wa abiria walionusurika, mwendo wake ulikuwa wa kawaida, huku mvua ikinyesha.

Abiria hao wamesema kabla ya kupinduka, basi hilo lilisereleka na kugonga gema kando ya barabara.

Mabasi ya Machame Investment huondoka jijini Dodoma saa 12 asubuhi kila siku, na huwasili mjini Moshi majira ya saa 12 jioni.

Post a Comment

0 Comments