PLO Lumumba ashauri kuundwa kwa East African Airline

Profesa wa sheria na mtoa mihadhara maarufu kutoka Kenya, Prof. PLO Lumumba ameshauri kuwa, ni vema mashirika ya ndege ya mataifa yanayounda jumuiya ya Afrika Mashariki kuunganisha nguvu na kuunda shirika moja la East African Airline, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.

Kwa mujibu wa PLO Lumumba, Kenya Airways, Air Tanzania, Uganda Airlines, Rwandaiar, Air Burundi wakijumuisha na Sudan ya Kusini wakiungana wanaweza kuunda shirika moja lenye nguvu ambalo litaweza kukabiliana na changamoto ya hasara zinazojitokeza kwa sasa.

"Serikali zinaweza kuchukua asilimia 10 ya hisa kwa kila mmoja na hiyo asilimia 40 iachwe kwa ajili ya umma,"ameeleza PLO Lumumba.

Wito huo unakuja ikiwa mwaka 1977 Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (East Africa Airways ) ambalo liliasisiwa mwaka Januari Mosi, 1946 lilivunjika.

Shirika hilo ambalo lilikuwa na makao yake makuu jijini Nairobi lilikuwa linaundwa na mataifa matatu tu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo ikiwemo Kenya, Tanzania na Uganda na ndilo shirika la ndege lililotumika hapo kabla kuhudumia jumuiya ya Afrika Mashariki.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wameieleza DIRAMAKINI kuwa, suala la hasara kwa mashirika ya ndege kwa sasa iwe ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki haiwezi kukwepeka kutokana na mwenendo ulivyo wa hali ya kiuchumi, kuzorota kwa shughuli za kitalii na magonjwa ambayo yamewakosesha fursa watu wengi kusafiri kama virusi vya Corona (COVID-19).

Post a Comment

0 Comments