Rais Samia apangua Baraza la Mawaziri, Dkt.Bashiru apewa Ubunge,Balozi Katanga ndiye Katibu Mkuu Kiongozi

Balozi wa Tanzania nchini Japan, Hussein Yahya Katanga ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dodoma).

Uamuzi huo ameufikia leo Machi 31, 2021 baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Isidor Mpango kuapishwa katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kuondoka kwa Dkt. Philip Mpango katika Wizara ya Fedha na Mipango kumempa nafasi ya kulitazama baraza lote la mawaziri na kufanya mabadiliko kidogo.

“Nimeona niwabadilishe kwa sababu tangu mmeapa ni muda mfupi kuona nani ameshindwa, tunaanza na hawa awamu ya sita, jinsi tunavyokwenda tutaona nani tunakwenda nae na nani tunamuacha,"amesema.

Mbali na uteuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Rais Samia amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri ambalo liliteuliwa na mtangulizi wake aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa tanzania, Hayati Dkt.John Magufuli ambaye alifariki Machi 17, mwaka huu akiwa katika matibabu Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam.

Rais Samia amemteua Balozi Hussein Yahya Katanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi akichukua nafasi ya Dkt.Bashiru Ally ambaye ameteuliwa kuwa Mbunge akiwa ndiye Katibu Mkuu Kiongozi aliyedumu madarakani kwa muda mfupi wa mwezi mmoja na siku nne.

Aidha, kupitia mabadiliko hayo Rais Samia Suluhu Hassan amemhamisha aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu kwenda Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Selemani Jafo akipelekwa kushika nafasi ya Ummy Mwalimu.

Dkt.Mwigulu Nchemba amepelekwa Wizara ya Fedha na Mipango akisaidiwa na Hamad Masauni na nafasi yake katika Wizara ya Katiba na Sheria imechukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Paramagamba Kabudi akisaidiwa na Jofrey Mizengo Pinda. Awali, Prof.Kabudi kabla ya Wizara ya Mambo ya Nje aliwahi kuhudumu katika wizara hii.

Kwa upande wake Balozi Liberata Mulamula ambaye ni Mbunge wa kuteuliwa ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki huku Naibu wake akiteuliwa kuwa Mbarouk Nassoro Mbarouk.

Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais,Utumishi na Utawala Bora ameteuliwa Mohamed Omary Mchengelwa na manaibu wake wakiwa ni Mwita Waitara pamoja na Deogratius Ndejembi huku aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo,Kapteni mstaafu George Mkuchika akipangiwa kazi nyingine katika ofisi ya Rais.

Aidha, Wizara ya Uwekezaji imerejeshwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kutolewa Ofisi ya Rais huku Geoffrey Mwambe akiteuliwa kuwa Waziri wa wizara hiyo na Prof. Kitila Mkumbo akipelekwa Wizara ya Viwanda na Biashara na Naibu wake akibaki aliyekuwepo awali Exaud Kigahe.

Kwa upande wake, Pauline Gekul ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, huku aliyekuwa naibu waziri wa wizara hiyo, Abdallah Ulega akipelekwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa naibu waziri. Awali aliwahi kuhudumu katika wizara hiyo

Mwanaidi Ally Hamis ameteuliwa kuwa naibu waziri wa pili katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto.

Katika upande mwingine, Rais Samia amefanya uteuzi wa wabunge watatu ambao ni Dkt. Bashiru Ally, Balozi Liberata Mulamula na Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk. Kwa mujibu wa Rais Samia mawaziri na manaibu wataapishwa Ikulu ya Chamwino kesho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news