Serikali yatenga bilioni 22.5/- kununua vifaa tiba na ajira za watumishi wa afya

Serikali imetenga shilingi bilioni 22.5 katika mwaka ujao wa fedha kununua vifaa tiba na kutoa ajira kwa watumishi wa kada ya afya ili kuweza kutosheleza mahitaji ya hospitali mpya za wilaya na vituo vya afya vipya 487 vilivyojengwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dodoma).
Akijibu swali la Mbunge wa Vwawa Mhe.Japhet Hasunga aliyetaka kujua ni lini serikali itapeleka vifaa tiba na watumishi wa afya kwenye kituo cha afya cha Ilula ambacho ujenzi wake ulikamilika miaka miwili iliyopita, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Mhe.Dkt Festo Dugange amesema kuwa serikali inatambua uhaba wa vifaa tiba na watumishi wa afya katika hospitali na vituo vya afya vilivyojengwa hivyo imetenga kiasi hicho cha fedha ili kununua vifaa tiba na kuajiri watumishi.

Amesema sambamba na kazi inayoendelea ya ujenzi wa vituo vipya vya afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI inatarajia kuomba takribani shilingi bilioni 22.5 kwa ajili ya kuhakikisha vituo vyote vya afya vilivyojengwa na hospitali zote za halmashauri zinapatiwa vifaa tiba na hili litafanywa kwa kushirikiana na mapato ya ndani ya halmashauri.

“Lakini pili mpango upo wa kwenda kuajiri watumishi ili kuwapeleka katika vituo hivi, hivyo naomba kumuhakikishia Mhe.Hasunga na wabunge wengine wenye hoja kama hizo kuwa serikali inazo takwimu za kutosha za mahitaji ya vifaa tiba katika vituo vyetu vya afya na mahitaji ya watumishi katika vituo hivyo, na itaajiri watumishi kadri ya upatikanaji wa fedha,” amesema.

Mapema, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum kutoka mkoa wa Songwe Mhe. Neema Gerald Mwangamila ambaye alitaka kujua ni lini Hospitali mpya ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma inatarajia kuanza kutoa huduma, Mhe.Dkt Dugange amesema hospitali hiyo mpya itaanza kutoa huduma za awali kwa wagonjwa wa nje ifikapo tarehe 27 aprili, 2021.

Amesema tayari serikali imetenga katika bajeti ijayo shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi na shilingi milioni 500 kwa ajili ya vifaa tiba.

Akijibu swali la Mbunge wa Ukerewe Mhe.Joseph Mkundi ambaye alitaka kujua ni lini kituo kipya cha afya cha Nakatunguru ambacho kimekamilika kujengwa kitapelekewa vifaa tiba na watumishi, Mhe. Dkt Dugange amesema tayari serikali imekwishapanga kupeleka watumishi wachache na vifaa tiba vilivyopo katika kituo hicho lakini katika mwaka wa fedha ujao imetenga fedha za vifaa tiba na kupeleka watumishi watakaoajiriwa katika kituo hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news