TAMKO LA PONGEZI KWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGAMO WA TANZANIA MH. SAMIA SULUHU HASSAN JUU YA KUFUNGULIWA KWA VYOMBO VYA HABARI VILIVYOFUNGWA

Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Mwanza(MPC), inachukua nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi yake ya kuagiza vyombo vya habari vyote vilivyokuwa vimefungiwa kwa sababu mbalimbali vifunguliwe na viendelee na dhima yake ya kutafuta na kuchakata taarifa na kusambaza habari kwa umma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia mara baada ya kuwaapisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi Ikulu jijini Dar es salaam Aprili 6, 2021

MPC inapongeza kwa dhati maamuzi ya Mhe. Rais kwani ni maamuzi yanayolenga kuruhusu vyombo vya habari kufanya kazi zake kwenye mazingira rafiki bila vikwazo.

MPC ina amini dhima ya vyombo vya habari ni kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha. Vyombo vya habari vinapokuwa huru vinafanya kazi zake kwenye mawanda mapana ya kuleta maendeleo kupitia fikra pevu za misingi ya uandishi wa habari.

Kitendo kilichofanywa na Rais ni kitendo cha hekima na busara kwa tasnia ya habari hapa nchini, MPC inaamini Mhe. Rais amesikia kilio cha vyombo vya habari kwa muda mrefu.

Aidha MPC inaamini kuwa, vyombo vya habari sio adui wa Serikali bali ni rafiki wa Serikali kwenye kuhakikisha vinafanya kazi zake kwa weledi na kuibua kasoro mbalimbali zinazoathiri utendaji wa Serikali ili hatua stahiki zichukulie pamoja na kasoro hizo zifanyiwe kazi na kuleta mabadiliko chanya nchini.

Hata hivyo MPC inatoa wito wa kufanyiwa marekebisho ya sheria mbalimbali zinazo ongoza taaluma ya habari nchini, ikiwemo Sheria ya Huduma ya vyombo vya habari 2016 kama iliyoamriwa na Mahakama ya Haki ya Afrika ya Mashariki pamoja na sheria nyingine na kanuni zenye ukakasi.

Mwisho MPC inatoa rai kwa Waandishi habari nchini kufanya kazi katika misingi ya weledi ili kushiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa Taifa letu kwani wajibu wa vyombo vya habari ni kujenga na sio kubomoa.

Edwin Soko

Mwenyekiti

MPC 

06.04.2020

Post a Comment

0 Comments