KWA SHAKA HAMDU SHAKA, CCM IMELAMBA DUME

Mwandishi Shaaban Robert aliandika katika ya moja ya vitabu vyake kuwa Dunia huwaficha watu wake wema hadi tukio kubwa linapotokea, yumkini Ndugu Shaka Hamdu Shaka, Katibu mpya wa itikadi na uenezi CCM Taifa ni miongoni katika hao, anaandika Emmanuel J. Shilatu.
Kwa maisha ya kisiasa na maisha aliyopitia yalikuwa ni kificho na changamoto tosha kwa Ndugu Shaka lakini siku zote alisimama imara.

Ngoja niwakumbushe baadhi ya mambo machache tu. Ndugu Shaka amekaa muda mrefu akiwa ni Kaimu Katibu Mkuu Jumuiya ya Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa pasipo kuthibitishwa rasmi kuwa Katibu Mkuu UVCCM Taifa lakini hatukuwahi kusikia akilalamika juu ya jambo hilo na badala yake alipambana vilivyo na kufanikiwa kumudu vyema majukumu yake na kuisimamisha vyema UVCCM na kufanya iwike vizuri kuliko Jumuiya nyingine, huyo ndio Shaka nimjuaye.

Hata wakati akiwa Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro alipita kwenye misukosuko mingi kutokana na upekee wa siasa za Morogoro lakini kwa utendaji wake Mkoa wa Morogoro ulipata nafasi za ubunge, udiwani nyingi za kupita bila kupingwa na kura nyingi za Urais CCM kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. 

Unapozungumzia Tanzania ya kijani ilianza kupepea vyema mkoa wa Morogoro ambapo Ndugu Shaka Hamdu Shaka alikuwa mtendaji mkuu (Katibu) wa chama (CCM) kimkoa.

Ndugu Shaka ni mmojawapo wa Vijana wachache wenye uweledi na maarifa zaidi juu ya siasa za Tanzania kwa kujua namna ya kucheza, kushiriki nazo kimkakati na kuleta ushindi kwa muda mrefu. 

Ndugu Shaka anazijua figisu, anajua kujenga hoja, anajua kupangua propaganda za wapinzani ipasavyo. Wa ufipa na wa Mtambwe Nyani wanamuelewa vyema Shaka ni nani juu ya masuala ya siasa, itikadi na uenezi.

Siri ya mafanikio ya Shaka ni subira, uvumilivu, utulivu, hekima, busara, upendo na kujishusha kwake kwa rika zote kwani hapendi ubaguzi kimakundi, kujisikia, dharau kama wengineo wapatapo dhamana kubwa.

Nyinginezo ni unyenyekevu, nidhamu, uzalendo, uadilifu, ufuatiliaji na uchapa kazi. Huyo ndio Shaka Hamdu Shaka nimjuaye.

Unapozungumzia ustawi wa demokrasia, uweledi na elimu ya siasa kwa wengine, siasa safi za kiushindani zenye tija na hoja, mikakati ya ushindi usioumiza wengine, uzoefu masuala ya kisiasa basi unamzungumzia Shaka Hamdu Shaka. Hakika CCM imelamba dume, Ndugu Shaka Hamdu Shaka.

Post a Comment

0 Comments