Massimiliano Allegri ateuliwa kuwa kocha wa Juventus, Andrea Pirlo atimuliwa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Baada ya kocha Andrea Pirlo kufutwa kazi wiki moja baada ya msimu kumalizika, Klabu ya Juventus imemteua aliyekuwa kocha wao, Massimiliano Allegri kuendeleza gurudumu.
Massimilano Allegri, kocha wa Juventus. (Picha na Skysports).

Pirlo ambaye ni raia wa Italia inaelezwa alikuwa chaguo lenye kushangaza katika kumpokea Maurizio Sarri mwishoni mwa msimu uliopita 2019/2020 na hata matokeo yake yakawa ya kushangaza.

Kocha huyo alishindwa kuipa ubingwa wa Serie A pamoja na kumaliza nafasi nne za juu kwa shida katika msimu.

Klabu ya Juventus wamekosa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012.

Ujio wa Allegri unaelezwa huenda ukarejesha matumaini kwani alikuwa kwenye nafasi ya ukocha mwaka 2014 hadi 2019 ambapo alifanikiwa kuipa mataji matatu ya Ligi ya nyumbani Serie A, Kombe la Coppa Italia mara nne na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa mara mbili.

Hatua hiyo inazima ndoto za awali, kwani Allegri alitajwa kuwa ndiye atajaza nafasi iliyoachwa wazi Real Madrid kufuatia kuondoka kwa Zinedine Zidane, lakini Antonio Conte, ambaye aliiongoza Inter Milan kutwaa taji la Serie A msimu uliopita, sasa inaaminika atachukuliwa mikoba ya Zidane huko Bernabeu. Zidane ang'atuka Real Madrid soma hapa.

Baada ya kurejea Allianz Stadium, taarifa iliyotolewa imeeleza kuwa, "Massimiliano Allegri ndiye meneja wa Juventus kwa mara nyingine. Allegri anachukua benchi ambalo analijua vizuri, klabu inayompenda na anayoipenda, kwani leo safari mpya tunaianza pamoja, kuelekea malengo mapya.

"Kile alichofanikiwa katika safari yake ya kwanza Juventus kimeandikwa katika historia ya klabu. Sasa tuko tayari kuanza maisha mapya na kocha Allegri,”imeeleza taarifa hiyo.

Ujio wa Allegri mwenye umri wa miaka 53 katika klabu ya Juventus unakuja baada ya kukaa benchi bila kazi tangu afutwe kazi Juni, 2019.

Aidha,Pirlo ambaye aliondolewa kazini Mei 28, 2021 akiwa na umri wa miaka 42, anatajwa kukosa matokeo bora hivyo kuifanya klabu hiyo kuyumba.

Post a Comment

0 Comments