Mbowe ataja mambo yanayowaumiza vichwa CHADEMA

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema, ushindani wa kisiasa hapa nchini upo katika vyama wiwili pekee na vyama vingine bado havina ushindani wa kweli katika kuleta mabadiliko ya dhati na yenye tija kwa Watanzania, anaripoti AMOS LUFUNGILO (Diramakini) Mara.
Amesema kuwa, wataendelea kuwa na msimamo wa dhati katika kudai mapinduzi ya kweli ya kimaendeleo kwa wananchi, hivyo hawatarudi nyuma kupigania suala la tume huru ya uchaguzi pamoja na kudai katiba mpya itakayoleta dira watanzania wote.

Mheshimiwa Mbowe ameyasema hayo akiwa Mjini Musoma mkoani Mara wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali kutoka chama hicho Kanda ya Serengeti na makao makuu.

Mbowe amesema, chama hicho kinataka katiba ambayo itawaweka viongozi madarakani kwa njia ya kupigiwa kura na wananchi badala ya kuteuliwa.

‘’Katiba ya sasa imempa majukumu mengi sana Rais, anachagua tume ya uchaguzi, wakurugenzi wa halmashauri ndiyo wanasimamia uchaguzi, wakuu wa mikoa na wilaya wanateuliwa na Rais hawawezi kutenda haki hata kidogo. Cha msingi chama tujiimarishe kikamilifu kwa kukijenga chama chetu,"amesema Mheshimiwa Mbowe.

Pia ameongeza kuwa, mchakato wa katiba katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu Dkt.Jakaya Kikwete ulitokana na CHADEMA kuishinikiza serikali kudai katiba mpya, akawataka wanachama wa chama hicho kushiriki vyema kukijenga chama hicho kwa umoja kwa lengo la kujenga chama cha mfano na cha kihistoria duniani.

Mheshimiwa Mbowe amewataka wanachama wa chama hicho kuanzia Julai Mosi, 2021 wanachama wote wataandikishwa upya kwa mfumo wa kidigitali kwa shilingi 2,500 kila mwanachama kuwezesha chama hicho kujijenga kiuchumi.

‘’Fedha hii itagawanywa katika maeneo mbalimbali kuanzia ngazi ya kata, wilaya na makao makuu asilimia 20 pekee ndiyo itabaki, lazima viongozi wa chama muwajibike kwa jambo hili fedha hizi zitanunua vifaa, magari ya chama na hata kusaidia matumizi ya ofisi na zitakuwepo kadi aina tano ambapo kadi ya kwanza shilingi 2,500, kadi ya pili 25,000, kadi ya tatu 50,000, kadi ya nne 100,000 na kadi ya tano shilingi 200,000,’’amesema Mbowe.

Mheshimiwa Mbowe ameongeza kuwa, chama hicho pia kitaanzisha CHADEMA Digital Saccos ili wanachama waweze kupata fursa ya mikopo na mpango huo utafuata baada ya kukamilika kwa usajili mpya wa wanachama kwa njia ya kidigitali.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Mbowe amesema kuwa, chama hicho lazima kiwe na ofisi zenye hadhi, hivyo lazima kijiimarishe kujenga majengo bora kwa kutumia fedha zao wenyewe pasipo kutegemea ruzuku kutoka sehemu yoyote ili kusonga mbele.

Post a Comment

0 Comments