Mwalimu Nkwama:Majalada ya walimu nchini yanaingizwa kwenye mfumo

Na Diramakini (diramakini@gmail.com)

JUMLA ya majalada 367,022 yanatarajiwa kuingizwa kwenye mfumo wa kielekroniki wa kuhifadhi kumbukumbu za waalimu unaoitwa E-Office ambapo mpaka sasa tayari majalada 20,000 yameingizwa kwenye mfumo huo yakiwemo ya upandishaji wa madaraja kwa walimu.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwalimu Paulina Nkwama katika ziara ya kikazi ya ufuatiliaji wa zoezi la upandishwaji wa madaraja kwa walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Nkwama amesema kuwa, Tume ya Utumishi wa Walimu imeanzisha mfumo huo ikiwa ni mbadala wa matumizi ya nakala ngumu.

Amesema kuwa, tume hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inaendelea kujiimarisha katika suala zima la mifumo ili kurahisisha utendaji kazi wa tume hiyo.

Nkwama amesema kuwa, TSC inaendelea kujiimarisha katika mifumo ya utendaji kazi ambapo mfumo wa E- office unasaidia katika kuhakikisha mafaili yote yakiwemo ya waalimu kupandishwa madaraja yanaingizwa kwenye mfumo na kufanyiwa kazi.

Aidha, ameweka wazi kuwasiliana na Ofisi hiyo kupitia tovuti ambayo ni www.tsc.go.tz, barua pepe secretary@tsc,go.tz na watasaidiwa kwa haraka zaidi.

Wakati huo huo, Mwalimu Paulina Nkwama ametoa rai kwa wilaya zote za Tume za Utumishi wa Walimu nchini kuhakikisha zoezi la upandishaji wa madaraja kwa waalimu kuanzia ngazi ya Sekretarieti ihakikishe inafanya kazi kwa kufuata muongozo, uliotolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora.

Pia amewataka kuhakikisha wanafanya zoezi hilo kwa weledi , ufanisi, haki na bila upendeleo lengo likiwa walimu wenye sifa wapande vyeo na ambao hawana sifa wajibidishe na kusubiri wakati mwingine.

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani kwa kuona umuhimu wa kutoa motisha kwa watumishi wa umma.

Aidha, amewataka walimu kuhakikisha wanafanya kazi kwa nguvu zao zote kwa kuwa ni wajibu wao kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha, weledi na ufanisi kwa kuhakikisha wanatoa elimu bora kwa wanafunzi.

Katibu Msaidizi Tume ya Utumishi wa Walimu Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni,Mwalimu Hawa Rajabu amesema kuwa wanategemea kupandisha vyeo waalimu 444 ambao wanasifa kulingana na muongozo uliotolewa wa upandishaji vyeo kutoka kwa Katibu Mkuu Utumishi.

Post a Comment

0 Comments