Yanga SC yafuzu nusu fainali Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania

Na Diramakini (diramakini@gmail.com)

Wanajangwani, Yanga SC wamefanikiwa kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Mwadui FC.

Ni kupitia kambumbu lililopigwa Mei 25,2021 katika Dimba la CCM Kambarage mjini Shinyanga. Kiungo Deus David Kaseke dakika ya 25 na 57 ndiye aliyeiwezesha Yanga SC kusonga mbele baada ya mabao yake mawili.

Kwa ushindi huo, Yanga SC wanatarajiwa kukutana na Wanajeshi wa mpakani timu ya Biashara United kutoka mkoani Mara ambayo iliiondosha Namungo FC.

Awali,katika mchezo huo uliokuwa wa kasi na kusisimua, timu ya Biashara United Mara ilipata bao la kwanza dakika ya 8 lililowekwa kimiani na mchezaji wake Mpapi Nasibu.

Mchezo uliendelea kwa kasi huku Biashara United Mara wakipambana kuongeza bao jingine na Namungo FC wakitaka kusawazisha.

Biashara United Mara waliweza kupata bao la pili lililofungwa na Kelvin Friday dakika ya 38 kwa mkwaju wa penati baada ya mcheziji wa Biashara United Mara, Tarick Simba kuchezewa madhambi eneo la hatari.

Hadi mchezo huo unakwenda mapumziko timu ya Biashara United Mara walikuwa mbele kwa mabao 2, huku timu ya Namungo FC wakiwa 0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikicheza kwa bidii na kufanya mabadiliko kuhakikisha kwamba inapata matokeo. Lakini safu za ulinzi za timu zote mbili zilikuwa imara kuzuia mashambulizi.

Hadi mchezo huo unamalizika Timu ya Biashara United Mara iliibuka na ushindi wa mabao 2-0. Robo fainali za mwisho za michuano hiyo, maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) zitachezwa kati ya Rhino Rangers na Azam FC katika dimba la Kambarage na Simba SC dhidi ya Dodoma Jiji FC katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments