CHADEMA yaibua mambo mawili, yataka yaingizwe kwenye bajeti

NA MWANDISHI DIRAMAKINI, Dar
 
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Mheshimiwa John Mnyika amesema kuwa, kuna kila sababu ya mipango ya Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi nchini kuingizwa katika bajeti.

Amesema, hatua hiyo ni muhimu zaidi katika kuyafikia haraka maendeleo ya Taifa ambayo yamekusudiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha.
Mheshimiwa Mnyika ameyasema hayo Juni 12, 2021 mkoani Dar es Salaam wakati akizungumzia kuhusiana na bajeti ya Serikali mwaka 2021/22 iliyosomwa bungeni siku mbili kabla ya ombi hilo.

Amesema, Katiba mpya ndio mradi muhimu kwa Taifa kwa sasa kwani itajenga misingi ya ujenzi wa Taifa kwa miaka zaidi ya hamsini ijayo.

Mheshimiwa Mnyika amesema kuwa,jambo la kipaumbele kuliko yote ni kufikiria kuandika Katiba mpya kwa sababu ndio mchakato muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Pia amewataka Watanzania kujadili kuhusu suala la Katiba mpya kama kipaumbele muhimu ambacho Serikali inapaswa kukifanyia kazi katika bajeti ya mwaka 2021/22.

Aidha, amesema wananchi wako tayari kutozwa kodi ya katiba mpya ili kufanikisha mchakato wa kuipata mapema.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Mnyika ameitaka Serikali kuziondoa kodi za laini ya simu na kodi ya majengo itakayolipwa kupitia mfumo wa Luku kwa madai kwamba zitawaumiza wananchi hasa wapangaji ambao watalazimika kulipia majengo yasiyokuwa mali zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news