Mbunge atimuliwa bungeni kwa suruali ya kuwatega waheshimiwa

Baada ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kumtaka Mbunge, Hussein Nassor Amar kumtaja Mbunge mmoja ambaye amemuona ndipo alipomtaja Mbunge wa Momba, Condester Michael Sichalwe ambapo Spika Ndugai alimtaka atoke ndani ya ukumbi wa bunge ili akabadilishe mavazi yake.

“Spika nasimama kwa kanuni ya 70 inayohusu mavazi ya staha kwa wabunge, kanuni imeeleza wazi kuhusu mavazi hayo na kwa akina dada, lakini humu ndani kuna wabunge wamevaa nguo ambazo hazina staha,”amesema Mheshimiwa Amar.
Mbunge wa Momba Condester Michael Sichalwe akitolewa ndani ya ukumbi wa bunge ili akabadilishe mavazi yake baada ya Mbunge wa Nyangw’ale, Hussein Nassor Amar kuomba muongozo wa Spika kuwa kuna baadhi ya wabunge wamevaa mavazi yasio na maadili.

“Mbunge huyo yuko hapo katika mkono wangu wa kulia, amevalia tisheti lakini naomba umuite mbele uone suruali aliyovaa namna ilivyobana, amevaa miwani,” amesema Amar.

Spika alisimama na kumtaka mbunge aliyevaa mavazi hayo asimame na aondoke ndani ya ukumbi ili akavae mavazi yenye staha ndipo atarejea tena bungeni.

Sichwale alisimama akabeba mkoba wake na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.

Spika Ndugai ameagiza askari wote katika milango ya kuingia bungeni wawe makini wasiruhusu wabunge kuingia wakiwa wamevaa mavazi yaliyokatazwa.

Post a Comment

0 Comments